Main Title

source : Parstoday
Jumamosi

6 Mei 2023

16:39:55
1363196

Profesa wa Chuo Kikuu US: Ziara ya Rais wa Iran Syria ni kiashiria cha ushindi wa Muqawama

David Yaghoubian, Profesa na mhadhiri wa Historia wa Chuo Kikuu cha Jimbo la California nchini Marekani amesema ziara ya rais wa Iran nchini Syria ni kiashiria cha ushindi wa mhimili wa Muqawama katika vita vichafu vya Syria vilivyoanzishwa kwa uungaji mkono na Marekani, ambapo Washington haikuweza kuleta mabadiliko ya utawala iliyokusudia ili kuigawa vipande vipande nchi hiyo.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ina ushirikiano wa kistratejia na Syria, na hilo limethibitishwa na uungaji mkono wa Tehran kwa serikali halali ya nchi hiyo wakati wote wa mgogoro wa Syria na kuisaidia serikali ya rais Bashar al-Assad katika harakati za kupambana na makundi mbalimbali ya kigaidi.Baada ya kushindwa kundi la kigaidi la DAESH (ISIS), uhusiano wa Syria na Iran hivi sasa umepanuka na kujumuisha nyuga mbalimbali, na kuna matarajio ya wazi ya kustawishwa uhusiano huo katika nyanja zote.Kwa mujibu wa shirika rasmi la habari la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran IRNA, Dk David N. Yaghoubian, Profesa wa historia katika Chuo Kikuu cha Jimbo la California, amesema kuhusu ziara ya Rais Ebrahim Raisi nchini Syria kwamba ziara hiyo imepanua wigo wa umoja wa kihistoria ambao umekuwa na ulazima kwa nchi hizo mbili katika nyakati za mgogoro mkubwa na vinapoibuka vitisho dhidi ya mamlaka ya kitaifa ya mataifa hayo.

Profesa Yaghoubian ameongeza kuwa Marekani haiungi mkono kurejeshwa uhusiano kati ya Syria na nchi zingine kwa sababu hatua hiyo ni kiashiria cha kushindwa rasmi vita vichafu vya Marekani dhidi ya Syria, ambapo mabilioni ya dola yalitumika kusaidia magenge ya kigaidi ya ukufurishaji yaliyokuwa na lengo la kuipindua serikali ya Syria, kuigawanya vipande vipande nchi hiyo na kuuweka madarakani utawala kibaraka utakaounga mkono utawala wa kibaguzi wa Israel na kuafiki kuporwa na utawala huo Miinuko ya Golan ya Syria.

Tarehe 3 Mei, Ayatullah Seyed Ebrahim Raisi, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, alitembelea Syria kwa mwaliko rasmi wa Rais Bashar al-Assad wa nchi hiyo akiongoza ujumbe wa ngazi za juu wa maafisa wa kisiasa na kiuchumi. Safari hiyo ni ziara ya kwanza ya rais wa Iran nchini Syria tangu mwaka 2011 ulipoanza mgogoro wa nchi hio.Katika ziara hiyo, maafisa waandamizi wa Iran na Syria walitia saini hati 14 za ushirikiano katika nyanja mbalimbali katika hafla iliyohudhuriwa na marais Raisi na  Assad.../

 342/