Main Title

source : Parstoday
Jumatano

10 Mei 2023

10:25:03
1364461

Trump ahukumiwa kulipa fidia ya dola milioni tano katika kesi ya unyanyasaji wa kingono

Baraza la Wazee la Mahakama ya Serikali Kuu katika jimbo la New York nchini Marekani imempata na hatia rais wa zamani wa nchi hiyo Donald Trump katika kesi ya unyanyasaji wa kingono na kumchafulia mtu jina na kumhukumu kulipa fidia ya zaidi ya dola milioni tano.

Kwa mujibu wa shirika la habari la IRNA, wajumbe wa Baraza la Wazee la Mahakama Kuu ya New York linalojumuisha wanawake watatu na wanaume sita walitangaza jana Jumanne kwamba Jane Carroll, mwandishi wa Kimarekani mwenye umri wa miaka 79 ameweza kuthibitisha madai yake kuhusu malalamiko ya mashtaka aliyowasilisha dhidi ya rais wa zamani Donald Trump  kwamba alimnyanyasa kingono ndani ya duka moja kuu mnamo mwaka 1996. Kwa sababu hiyo, Trump mwenye umri wa miaka 76 ametakiwa alipe fidia ya zaidi ya dola milioni tano. Jopo hilo la wazee wa Mahakama limethibitisha pia maelezo ya Carroll kwamba rais huyo wa zamani wa Marekani alimchafulia jina kwa kumuita mwongo mnamo Oktoba 12, 2022, kupitia ujumbe mrefu aliomtumia kwenye ukurasa wake Trump wa kijamii wa Truth Social.

Mnamo Aprili 25, mahakama hiyo ya serikali kuu mjini New York ilianza kusikiliza mashtaka ya madai ya Bi. E. Jane Carroll aliyefungua kesi dhidi ya Trump akidai kwamba rais huyo wa zamani wa Marekani alimbaka katika duka kubwa la jiji la New York katika miaka ya 1990.

 Trump alitaja madai ya mwanamke huyo kuwa ni "utapeli", "udanganyifu" na "uongo mtupu". Kauli hizo za rais huyo wa zamani wa Marekani zilimfanya Carroli amshitaki kwa kumchafulia jina pia na kumtusi, lakini Trump anaamini kuwa kauli zake si za matusi na kwamba alichofanya ni kueleza ukweli. Kesi hiyo ni pamoja na kesi nyingine ambayo Trump alishtakiwa mapema mwezi uliopita ya tuhuma za kughushi rekodi za kibiashara na kutoa malipo ya siri ya kizibamdomo kwa nyota wa filamu za ngono.Mnamo Aprili 4, rais huyo wa zamani wa Marekani alifika mbele ya mahakama ya Manhattan akikabiliwa na shtaka la ufichaji mambo na kulipa kizibamdomo kwa Stormy Daniels, mwigizaji wa filamu za ngono kabla ya uchaguzi wa 2016 anayesemekana kwamba alikuwa na mahusiano naye haramu ya kingono wakati yeye Trump yuko katika ndoa. Trump anajiandaa kujitosa kwenye kinyang'anyiro cha kuwania kuingia tena Ikulu ya White House mnamo mwaka 2024 na anaonekana na wengi kama ndiye mgombea mteule wa chama cha Republican.../

342/