New Zealand, Kanada, Australia, Uingereza, Ufaransa, Venezuela na Uruguay kila moja zimehimiza raia wao kuchukua tahadhari kubwa wakati wanapotembelea Marekani, kutokana na vurugu za bunduki katika nchi hiyo.
Katika wikendi ya kwanza ya Mei, watu wanane walipigwa risasi na kuuawa katika jumba lenye shughuli nyingi la eneo la Dallas baada ya mtu mwenye bunduki mwenye umri wa miaka 33 kufyatua risasi kiholela na kuwajeruhi takriban wengine saba kabla ya kuuawa kwa kupigwa risasi na polisi.
Aidha wikendi iliyotangua huko Oklahoma, mbakaji aliyewahi kufungwa jela alimpiga risasi na kumuua mkewe, watoto wake watatu, na marafiki zao wawili kabla ya kujiua.
Hali kadhalika siku mbili tu kabla ya hapo, mwanamume mmoja aliwapiga risasi na kuwaua majirani watano, akiwemo mvulana wa miaka 9, baada ya kutakiwa aache kufyatua risasi hewani kiholela kwani kulikuwa na mtoto mchanga aliyekuwa akijaribu kulala. Mshukiwa wa kumpiga risasi alikamatwa baada ya msako uliodumu kwa siku kadhaa.
Kwa mujibu wa Jalada la Ghasia za Bunduki, Kumekuwa na visa zaidi ya visa 200 vya ufyatuaji risasi kwenye halaiki nchini Marekani hadi mwaka huu wa 2023.
Jarida hilo linafafanua ufyatuaji risasi kwenye halaiki kama tukio ambapo watu wanne au zaidi hujeruhiwa au kuuawa, bila kujumuisha mpiga risasi. Ingawa idadi ya ufyatuaji risasi ilipungua kidogo mnamo 2022, tangu 2018 ufyatuaji risasi kwenye halaiki umeongezeka kwa karibu 100 kila mwaka. Takwimu zinaonyesha kuwa, katika kila moja ya miaka mitatu iliyopita, kumekuwa na zaidi ya visa 600 vya ufyatuaji risasi kwenye halaiki nchini Marekani, au karibu visa viwili kila siku.
Tishio la utumiaji bunduki kiholela pamoja na ukosefu wa usalama nchini Marekani linazidi kuonekana kama tishio kubwa kwausalama kwa raia wa Marekani na watalii wanaotarajiwa.
Fahirisi ya Amani ya Ulimwengu ya 2022, ambayo hupima utulivu wa nchi na inajumuisha viashirio 23 vya ubora, inaorodhesha Marekani katika nafasi ya 129 kati ya nchi 163, na hivyo kuifanya kuwa miongoni mwa nchi hatari zaidi za kuishi duniani.
Katika mwaka 2022 pekee watu 20,128 waliuawa kote Marekani kwa kupigwa risasi katika matukio ya uhalifu huku makumu ya maelfu ya wengine wakijeruhiwa na kuachwa vilema.
342/