Main Title

source : Parstoday
Jumamosi

20 Mei 2023

14:08:46
1367236

Watu milioni 4.5 wapoteza maisha kutokana na ubabe wa kivita wa Marekani tangu 2001

Taasisi moja ya wasomi ya Marekani imetangaza baada ya kufanya utafiti wa kina na wa muda mrefu kwamba mamilioni ya watu katika maeneo ya Asia Magharibi (Mashariki ya Kati) na Afrika Kaskazini wamepoteza maisha tangu 2001 kutokana na uchochezi wa kivita wa Marekani.

Kulingana na utafiti huo uliofanywa na taasisi ya Watson yenye uhusiano na Chuo Kikuu cha Brown cha nchini Marekani, takriban watu milioni 4.5 wameuawa katika maeneo ya Asia Magharibi na Afrika Kaskazini kutokana na vita vilivyoanzishwa na Marekani baada ya 2001.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, kati ya idadi hiyo, watu wasiopungua milioni 3.6 hadi 3.7 wamekufa kutokana na athari za vita, ikiwa ni pamoja na kuporomoka uchumi, kupoteza usalama wa chakula, uharibifu wa miundombinu ya afya, uchafuzi wa mazingira na madhara mengine ya vita.

Takwimu hizo zimetolewa katika hali ambayo idadi halisi ya wahanga wa vita vya baada ya Septemba 11, 2001 imekuwa ikijadiliwa kwa mapana na marefu na kutiliwa shaka.

Mwaka 2015, Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka lilitangaza katika ripoti kwamba zaidi ya watu milioni moja waliuawa katika vita vilivyoanzishwa na Marekani katika nchi za Iraq, Afghanistan na Pakistan.

Hata hivyo, si rahisi kubainisha kwa usahihi idadi ya vifo visivyo vya moja kwa moja vilivyotokana na vita hivyo, ambapo vingi vilitokea kutokana na njaa na ukosefu wa usalama wa chakula, suala ambalo kwa kawaida hudhihiri baada ya miezi au hata miaka kadhaa baada ya kumalizika vita.

Katika uchunguzi wao, watafiti wamechukulia vifo vinne visivyo vya moja kwa moja kuwa sawa na kifo cha mtu mmoja katika vita vya kawaida, jambo ambalo limefanyika zaidi katika vita vya Yemen na Afghanistan kuliko Iraqi.

Ripoti ya Taasisi ya Watson inasema: "Vifo visivyo vya moja kwa moja husababisha uharibifu mkubwa, hasa ikitiliwa maanani kwamba uharibifu huo ungeweza kuzuiwa kama vita havingetokea. Rekodi ya vita vya Marekani dhidi ya kile kinachoitwa kuwa vita dhidi ya ugaidi imekuwa na matokeo mabaya kwa watu wa Mashariki ya Kati, Afrika Kaskazini na Asia ya Kati."

Rais George W. Bush wa Marekani, kwa kisingizio cha kulipiza kisasi mashambulizi ya Septemba 11, alitumia mbinu ya uchokozi na hujuma na kuzishambulia Afghanistan na Iraq kwa kisingizio cha mapambano ya kimataifa dhidi ya ugaidi.

Katika vita hivyo, zaidi ya watu milioni moja walipoteza maisha katika nchi za Iraq, Afghanistan, Syria, Libya na Yemen.

Ukaliaji wa mabavu wa Iraq na matokeo yake hatimaye ulipelekea kuundwa kwa makundi ya kigaidi kama Daesh, ambayo yalifanya uhalifu na jinai kubwa nchini Iraq na Syria. Kwa mujibu wa ripoti ya Watson, zaidi ya watu 906,000, ikiwa ni pamoja na raia 387,000, waliuawa moja kwa moja katika vita vya baada ya Septemba 11. Watu wengine milioni 38 walihama makazi yao au kulazimika kuwa wakimbizi.

Pia, mwezi Mei 2020, muungano unaoongozwa na Marekani dhidi ya Daesh ulikiri katika taarifa yake kwamba tangu mwaka 2014, uliua zaidi ya raia 1,300 huko Iraq na Syria, idadi ambayo hata hivyo ilitiliwa shaka na mashirika huru na ya kutetea haki za binadamu.

Kulingana na mashirika hayo, zaidi ya raia 1,600 waliuawa wakati wa kukombolewa mji wa Raqqa kutoka mikononi mwa magaidi wa Daesh mnamo 2017, ambapo zaidi ya asilimia 90 ya mji huo iliharibiwa kwa mashambulio makali ya anga na mizinga ya Marekani.

Pamoja na hayo lakini bado Marekani haikujifunza kutokana na chokochoko zake hizo za kivita hadi pale iliposhindwa kabisa  na hatimaye kulazimika kutoka kwa madhila nchini Afghanistan mwaka 2021.

James Dobbins, mchambuzi wa mambo katika Taasisi ya RAND, anasema: Ingawa kuna ukosoaji mkubwa unaofanywa kuhusu hatua ya Marekani ya kujiondoa Afghanistan, lakini wengi wanaamini kuwa uingiliaji wa Marekani nchini Afghanistan haukuwa sahihi, ulifanyika kimakosa na ulitarajiwa kufeli tangu mwanzo.

Pamoja na hayo lakini bado Washington inaendelea kuweka askari wake huko Iraq na Syria.

Mbali na kuwa vita hivyo vinaendelea kuua na kujeruhi maelfu ya wanajeshi wa Marekani, pia vinaongeza gharama kubwa katika bajeti ya nchi hiyo, ambayo kwa mujibu wa Donald Trump, rais wa zamani wa Marekani, inafikia dola trilioni saba.

Ripoti hiyo inaeleza kwamba serikali kuu ya Marekani imetumia zaidi ya dola trilioni nane katika vita hivyo vya uchokozi na ubabe.

Ni wazi kuwa washindi wakuu wa hatua za kijeshi za Marekani baada ya tukio la Septemba 11 ni makampuni ya kutengeneza silaha ya nchi hiyo. Kwa mujibu wa utafiti wa taasisi ya Watson, nusu ya bajeti ya Wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon) kati ya mwaka 2001 na 2020, ambayo ni dola trilioni 14, ilikwenda kwa wakandarasi na makampuni ya silaha ya nchi hiyo. Kati ya kiasi hicho, dola trilioni 4.4 zilikwenda kwa tasisi za kijeshi na kiviwanda za Marekani.

Mwanahistoria wa kimataifa na mchambuzi Charles Strozier anasema: Mashambulizi ya Septemba 11 yaliibua mgogoro mkubwa wa uwepo nchini Marekani, ambapo Washington iliyajibu mashammbulizi hayo kama "mnyama aliyejeruhiwa" kwa kuanzisha vita vya kinamasi dhidi ya ugaidi na hivyo kuharakisha kutokomea kwake yenyewe kama nguvu kuu duniani.

342/