Main Title

source : Parstoday
Jumamosi

20 Mei 2023

14:10:06
1367238

Newsweek: Biden ameshindwa katika vita kubwa zaidi nchini Syria

Jarida la Marekani la Newsweek limekutaja kurejea Syria kwenye Jumuiya ya Nchi za Kiarabu kuwa ni kushindwa kukubwa zaidi kwa Washington katika vita vya Syria.

Newsweek liliandika siku ya Alhamisi kuwa: Sera ya Joe Biden kuhusu Syria imepata pigo kubwa zaidi hadi sasa.

Wanadiplomasia wa Marekani wamekiri katika mahojiano na Newsweek kwamba "kurejea Damascus kwenye Jumuiya ya Nchi za Kiarabu (Arab League) kuna ujumbe muhimu kwa Marekani, nao ni mwisho wa uwepo wa kijeshi na kuondolewa kwa vikwazo vinavyoilenga nchi hiyo."

Kuhusiana na suala hilo duru za ujumbe wa Syria katika Umoja wa Mataifa zimesema katika mahojiano na jarida la Newsweek kuwa: “Msimamo wa Syria kuhusiana na kuwepo kinyume cha sheria askari wa Marekani katika baadhi ya maeneo ya ardhi ya nchi hiyo na hatua za upande mmoja zilizochukuliwa na Washington dhidi ya wananchi wa Syria, ni thabiti na zinazingatia kanuni na sheria ya kimataifa.

Itakumbukwa kuwa Rais Bashar al Assad wa Syria jana alishiriki kwa mara ya kwanza katika mkutano wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu mjini Jeddah nchini Saudi Arabia baada ya muongo mzima wa njama za kuitenga Syria. Kushiriki Rais wa Syria kwenye kikao hicho kumetajwa kuwa ni ushahidi wa kufeli njama zote za kikanda na kimataifa dhidi ya taifa hilo la Kiarabu.

Taarifa ya mwisho ya wakuu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu imesisitiza udharura wa kuheshimu maadili na tamaduni zingine na kuheshimu mamlaka, kujitawala na ardhi ya nchi mbalimbali, na vilevile kutounga mkono uundaji wa makundi ya waasi na ya wanamgambo.

342/