Main Title

source : Parstoday
Jumatatu

22 Mei 2023

05:03:51
1367680

Umoja wa Mataifa wataka mabadiliko Baraza la Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa, umewadia wakati wa kulifanyia marekebisho Baraza la Usalama la umoja huo pamoja na mfumo wa ubadilishaji wa fedha ulimwenguni ili viendanane na hali ya ulimwengu wa sasa.

Antonio Guterres amesema hay oleo katika mkutano na waandishi wa habari mjini Hiroshima, Japan, kunakofanyika mkutano wa kilele wa kundi la mataifa 7 tajiri.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameeleza kuwa, taasisi zote mbili zimekuwa zikiakisi mahusiano ya kimamlaka ya mwaka 1945, hivyo zinahitaji maboresho.

Aidha ameongeza kuwa, mfumo wa kifedha wa kimataifa umepitwa na wakati na hauna usawa.

Vilevile amesisitiza kuwa, kutokana na matukio ya ghafla ya janga la UVIKO-19 pamoja na vita vya Ukraine, mfumo huo umeshindwa kutimiza majukumu yake ya msingi kimataifa.

Kuweko mabadiliko katika mfumo wa sasa wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kilio cha muda mrefu hasa kutoka kwa mataifa ya Afrika.

Itakumbukwa kuwa, wakati wa mazungumzo ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuhusu mageuzi ya Baraza la Usalama mnamo Novemba 2022, wawakilishi wa Afrika walitoa wito wa kupanuliwa zaidi taasisi hiyo na uwepo wa Afrika kati ya wanachama wa kudumu na wasio wa kudumu wa Baraza la Usalama.

Viongozi mbalimbali barani Afrika wamekuwa wakilalamikia dhulma katika muundo wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na wamekuwa wakisisitiza kwamba, Afrika inapaswa kwa akali kuwa na mwanachama mmoja wa kudumu katika baraza hilo ambaye atakuwa na haki ya kura ya veto

Hivi karibuni pia Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa aliunga mkono wito wa kutolewa kiti cha kudumu cha Baraza la Usalama kwa bara la Afrika.

342/