Main Title

source : Parstoday
Jumanne

23 Mei 2023

10:56:27
1368081

Kulalamikia vikali Waislamu Kanada sheria mpya ya marufuku ya kusali shuleni

Waislamu nchini Kanada wamelalamikia vikali marufuku ya kusali iliyowekwa katika shule za serikali kwenye jimbo la Quebec.

Kwa mujibu wa amri ya Waziri wa Elimu wa jimbo la Quebec nchini Kanada, ni marufuku kwa vijana wa Kiislamu kutekeleza faradhi yao ya Swala katika skuli za serikali za jimbo hilo.

Madola ya Magharibi licha ya kutoa nara za usawa na haki za binadamu, lakini yamekuwa yakiongoza katika kukandamiza na kukiuka haki za binadamu kiasi kwamba, jamii za waliowachache au hata wafuasi wa dini za waliowachache hazina uhuru kabisa katika mataifa hayo. Jamii za waliowachache katika mataifa hayo zimekuwa zikibinywa na kukandamizwa kwa kila namna na hazina uhuru kabisa hata wa kuchagua aina ya nguo ya kuvaa, kutekeleza ibada zao na shughuli zao za kidini. Mfano wa karibuni kabisa wa ukandamizaji ni huu uliotokea katika jimbo la Quebec nchini Kanada wa marufuku kwa vijana wa Kiislamu kutekeleza faradhi yao ya Sala katika skuli za serikali za jimbo hilo.

Waislamu wa Kanada wamewasilisha malalamiko yao dhidi ya uamuzi huo na kusisitiza kwamba kupiga marufuku watu kusali katika skuli za serikali za Quebec kunapingana na Katiba ya nchi hiyo.

Jumuiya za Kiislamu nchini Kanada zimeitaka mahakama itangaze kwamba uamuzi uliochukuliwa na maafisa wa jimbo la Quebec umekiuka katiba ya nchi.

Taasisi sita, ikiwa ni pamoja na Jumuiya ya Kiislamu ya Kanada na Taasisi ya Waislamu wa Kanada, pamoja na asasi zingine nne za jimbo hilo, zimewasilisha kesi ya kutaka Mahakama ya Juu ya Quebec itangaze kuwa amri iliyotangazwa na jimbo hilo haitekelezeki au iifute.

Asasi hizo zimesisitiza kuwa agizo hilo ni la kibaguzi na linakiuka Mkataba wa Haki na Uhuru wa Kanada.

Katika hali ambayo kunapasiswa sheria kama hiyo ya kibaguzi katika jimbo la Quebec, Waislamu wa miji na majimbo mengine ya Kanada nao wamo katika mashinikizo makali. Hali hiyo imeshadidi kiasi cha kuifanya Kamati ya Bunge la Seneti la Canada kutangaza katika ripoti yake kwamba, chuki dhidi ya Uislamuu (Islamophobia) zimekita mizizi katika jamii ya Kanada na wanawake wanaojistiri kwa vazi la heshima la hijabu ndio walio hatarini zaidi.

Ripoti ya Kamati ya Haki za Binadamu ya Bunge la Seneti la Marekani inaeleza kwamba, makundi yenye chuki ya mrengo wa kulia yenye misimamo ya kufurutu ada na yaliyo dhidi ya Waislamu ambayo yamekuwa yakitekeleza vitendo vya chuki dhidi ya Waislamu yako katika hali ya kuongezeka na kuchukua wigo mpana zaidi.

Nchini Kanada Waislamu wa nchi hiyo hawaandamwi na ubaguzi katika masuala ya kidini tu, bali wanateseka kwa ubaguzi hata katika maeneo ya kazi. Utafiti mpya uliofanywa na Taasisi ya Islamic Relief unaonyesha kuwa, zaidi ya theluthi mbili ya Waislamu wa Kanada wanakabiliwa na vitendo vya kibaguzi katika maeneo yao ya kazi. Ufikiaji usio sawa wa vyeo, haki za kazi na majukumu au sera za kibaguzi kama vile kanuni za mavazi na sheria za kiofisi ni miongoni mwa ubaguzi huu.

Mbali na Kanada, Waislamu katika mataifa mengine ya magharibi wanakabiliwa na mazingira kama hayo hayo. Kuanzishwa wimbi la chuki dhidi ya Uislamu hususan katika miaka ya hivi karibuni ni jambo liliyoyafanya maisha ya Waislamu katika mataifa ya bara Ulaya kukabiliwa na matatizo chungu nzima. Madola ya Magharibi ambayo daima yamekuwa yakipigia upatu demokrasia na usawa, kivitendo yamekuwa wakiukaji wakuu wa haki za binadamu na hata kuuendesha waziwazi kampeni za chuki na ubaguzi dhidi ya Waislamu na jamii nyingine za waliowachache.

Massoud Shajareh, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Kimataifa ya Haki za Binadamu za Kiislamu (IHRC) yenye makao yake London nchini Uingereza anasema kuhusiana na jambo hili kwamba: Waislamu wanaoishi nchini Uingereza wanahesabiwa kuwa raia wa daraja la pili katika maeneo yote, ambapo hii ni natija ya kampeni ya chuki dhidi ya Uislamu ambazo zimekita mizizi katika utamaduni wa nchi hiyo.

342/