23 Mei 2023 - 11:00
Safari ya Rais Ebrahim Raisi Jakarta; fursa ya kuimarisha mashirikiano ya Iran na Indonesia

Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran leo ameelekea Jakarta, mji mkuu wa Indonesia akijibu mwaliko wa Rais wa nchi hiyo Joko Widodo al-maarufu Jokowi.

Lengo la safari hiyo ni kustawisha na kuimarisha zaidi ushirikiano wa kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni baina ya mataifa haya mawili muhimu katika ulimwengu wa Kiislamu.

Kukutana na kufanya mazungumzo na mwenyeji wake Rais Widodo na kutiwa saini hati kadhaa za ushirikiano baina ya Iran na Indonesia katika nyuga mbalimbali imetajwa kuwa sehemu ya ratiba ya Rais Ebrahim Raisi nchini Indonesia. Katika safari yake hiyo, Rais Ebrahim Raisi anatarajiwa kukutana na kufanya mazungumzo na Maspika wa Bunge la Wawakilisha na la Ushauri, wafanyabiashara na wadau wa masuala ya kiuchumi, Maulamaa na wanafikra wa Kiindonesia.

Safari hii inaweza kuwa ishara ya wazi ya kufunguliwa ukurasa mpya katika mahusiano ya Iran na Indonesia. Weledi wa mambo wanaamini kuwa, uhusiano mzuri wa kisiasa, mashirikiano ya kiuchumi na uwezo wa kiuchumi katika nyanja mbalimbali ni mambo ambayo yameandaa mazingira mwafaka ya kupanuliwa ushirikiano baina ya pande mbili.

Uhusiano wa kidiplomasia unaingia katika muongo wa 80 katika hali ambayo mahusiano ya mataifa mawili yana mizizi mirefu na imara katika historia; Wananchi wa mataifa haya mawili kwa karne nyingi  wakiwa Waislamu waliweza kuleta mafungamano imara na madhubuti baina yao; na Maulamaa na wanafikra wa Kiislamu wa Indonesia  na Iran walikuwa na ushirikiano mtawalia katika karne za huko nyuma.

Iran na Indonesia pia zina misimamo ya pamoja na inayokaribiana kuhusiana na masuala ya kieneo, kimataifa na katika ulimwengu wa Kiislamu na mahusiano ya pande mbili katika uga huu yanaendelea kushuhudiwa. Kwa mfano Marais wa Iran na Indonesia tarehe ya mwezi uliopita wa Aprili, walifanya mazungumzo kwa njia ya simu na kusisitiza juu ya udharura wa kuitishwa kikao cha Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) kwa ajili ya kujadili matukio ya Palestina na kile kinachoendelea katika ardhi hizo zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni maghasibu.

Hapana shaka kuwa, katika fremu ya vipaumbele katika sera zake za kigeni, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran sambamba na kuzingatia suala la kustawisha uhusiano wake na mataifa ya Kiislamu, inalipa umuhimu maalumu suala la kupanua ushirikiano wake na Indonesia ambayo ndio nchi ya Kiislamu yenye idadi kubwa zaidi ya watu. Indonesia nayo kwa upande wake katika mipango yake ya kiuchumi inatutafua masoko mapya kwa ajili ya kuwa na machaguo mengi ya kusafirisha bidhaa zake nje ya nchi na matokeo ya hilo ni kupunguza utegemezi kwa washirika wa jadi wa kibiashara.

Ni kwa kuzingatia ukweli huo wa mambo ndio maana viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Indonesia wameazimia kwa dhati kuandaa miundombinu na suhula hitajika kwa ajili ya kustawisha uhusiano wao katika nyanja mbalimbali. Uwepo na Iran na Indonesia katika baadhi ya asasi za kimataifa nayo ni fursa ya ushirikiano ambayo nayo ina nafasi muhimu katika kuimarisha uhusiano baina ya mataifa haya mawili muhimu ya Kiislamu.

Hata hivyo licha ya kuweko uhusiano mzuri kiasi hicho baina ya Iran na Indonesia, lakini kiwango cha mabadilishano ya kibiashara ni kidogo na ni kinyume kabisa na matarajio. Katika safari ya Rais wa Indonesia nchini Iran mwaka 2016 mataifa haya yalijiwekea malengo ya mabadilishano ya kibiashara yenye thamani ya dola bilioni mbili. Hata hivyo hadi sasa kiwango cha mabadilishano ya kibiashara baina ya mataifa haya mawili hakijavuka dola bilioni moja.

Kwa muktadha huo, safari ya Rais wa Iran nchini Indonesia pamoja na ujumbe aliofuatana nao, ni fursa mwafaka kwa ajili ya sekta za serikali na binafsi za nchi mbili kwa ajili ya kustawisha mahusiano na mashirikiano ya kiuchumi na kibiashara.

342/