Main Title

source : Parstoday
Jumatano

24 Mei 2023

11:14:51
1368416

Umuhimu wa ziara ya rais wa Iran nchini Indonesia

Rais Seyed Ebrahim Raisi, wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Jumatatu alitembelea Indonesia, kwa mwaliko rasmi wa rais mwenzake wa Indonesia, Joko Widodo.

Ziara ya Raisi nchini Indonesia ni ziara ya kwanza rasmi na ya kipekee ya marais wa Iran nchini humo tangu mwaka 2006. Katika kipindi cha miaka 17 iliyopita, marais wa Iran wametembelea Indonesia, lakini safari hizo zilikuwa za kushiriki katika mikutano ya kikanda na kimataifa. Safari hii maalumu nchini Indonesia inaenda sambamba na sera za kigeni za Iran, ambazo zinafuatiliwa kwa kuzingatia maendeleo ya kuwa na uhusiano mwema na nchi jirani, za kieneo na za Kiislamu.

Ziara ya Raisi nchini Indonesia ina maana kwamba maingiliano ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na nchi za Mashariki hayaishii China na Russia pekee, bali pia yanajumuisha nchi nyingine muhimu na zenye ushawishi mkubwa kama vile Indonesia, ambayo ni nchi kubwa ya Kiislamu yenye wakazi wapatao milioni 239.

Umuhimu mwingine wa safari ya Raisi nchini Indonesia unahusiana na ukweli kwamba safari hii inaonesha kushindwa kwa mkakati wa nchi za Magharibi hususan Marekani wa kutaka kuitenga Iran. Kwa hakika safari hii imebatilisha dhana potofu ya nchi za Magharibi kuhusu kutengwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Bila shaka, jambo muhimu zaidi katika ziara ya rais wa Iran nchini Indonesia linahusiana na uchumi. Indonesia ni mwanachama wa Kundi la G20  ambalo linajumuisha nchi zinazoibuka kiuchumi duniani. Nchi hii imepata ukuaji wa uchumi wa takriban asilimia 5 katika miongo miwili iliyopita. Shirika la Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo limekadiria kuwa uchumi wa Indonesia utakuwa wa nne mkubwa duniani ifikapo 2045.

Ingawa Indonesia ina akiba ya mafuta ghafi ya petroli inayokadiriwa kuwa mapipa bilioni 22, lakini maendeleo ya uchumi wa nchi hiyo hayatokani na mapato ya mafuta. Hivi sasa Indonesia ni moja ya nchi chache za Kiislamu ambazo zina mauzo ya nje ya bidhaa kubwa za kiviwanda na kisayansi. Siku hizi, Jakarta sio tu ni mji mkuu wa Indonesia, bali pia ni kitovu cha teknolojia nyingi mpya. Indonesia inashika nafasi ya kati ya nchi za Kusini-mashariki mwa Asia katika nyanja za teknolojia ya satelaiti. Nchi hii ya Kiislamu imerusha satelaiti 18 katika anga za mbali kwa madhumuni mbalimbali katika kipindi cha miaka minne pekee. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inahitaji uzoefu na uwezo wa Indonesia wa sayansi, uchumi na teknolojia na inaweza kuwa soko zuri kwa mauzo ya nje ya Indonesia.

Wakati huo huo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imepata uwezo mzuri wa ndani licha ya vikwazo vikubwa vya nchi za Magharibi katika uga wa teknolojia ya matibabu na dawa, na soko kubwa la Indonesia linaweza kuwa mnunuzi mzuri wa bidhaa hizo. Aidha mazulia, pistachio, tende, zafarani, kazi za mikono na dawa zinazotokana na mimea ni miongoni mwa bidhaa zingine zinazouzwa nje ya Iran kwenda Indonesia.

Ukweli mchungu kuhusu uhusiano wa Iran na Indonesia unahusiana na kiwango kidogo cha biashara kati ya nchi hizi mbili. Katika taarifa yake, Wizara ya Biashara ya Indonesia ilitangaza kuwa kiwango cha biashara kati ya Iran na Indonesia katika robo ya kwanza ya mwaka huu kilikuwa cha dola milioni 54.1, huku uhusiano wa kibiashara kati ya nchi hizi mbili ukiongezeka kwa asilimia 23 ikilinganishwa na mwaka uliopita  na kufika dola milioni 257.

Kwa kuzingatia uwezo uliotajwa wa nchi hizi mbili na pia kwa kuzingatia dhamira kubwa ya serikali za pande mbili ya kuendeleza uhusiano, inaweza kutarajiwa kuwa matokeo makuu ya ziara ya Rais Ebrahim Raisi nchini Indonesia yatakuwa ni kupanuka ushirikiano wa kiuchumi na kuongezeka kiasi cha biashara cha nchi hizi mbili.


342/