Main Title

source : Parstoday
Jumapili

28 Mei 2023

19:47:16
1369411

Mwaka wa tatu wa mauaji ya George Floyd; kuendelea ubaguzi wa rangi dhidi ya Wamarekani wenye asili ya Afrika

Ikiwa umetimia mwaka wa tatu tangu kuuawa kikatili George Floyd, Mmarekani mwenye asili ya Afrika, yaliyofanywa na polisi mbaguzi mzungu anayeitwa Derek Chauvin katika mji wa Minneapolis, Minnesota, suala la ubaguzi wa rangi na ukatili wa polisi nchini Marekani dhidi ya watu weusi au wenye asili ya Afrika bado ni miongoni mwa matatizo makubwa katika nchi hiyo.

Ubaguzi wa rangi na unyanyasaji dhidi ya watu weusi ni wa zamani na uliibuka wakati Marekani ilipoundwa kama nchi na daima umekuwa ukichukuliwa kuwa moja ya mambo yanayochukiza katika jamii ya Marekani.

Moja ya vipengele muhimu vya mgogoro huu wa ubaguzi rangi, ambao umeshadidi katika miaka ya hivi karibuni, ni unyanyasaji usio na kikomo wa polisi ya Marekani dhidi ya watu weusi au wenye asilia ya Afrika, ambao umezua matukio ya kusikitisha. Kwa mujibu wa takwimu, uwezekano wa watu weusi kuuawa na polisi nchini Marekani ni mara tatu ya ile ya watu weupe.

Kwa hakika, ubaguzi wa rangi na ukatili katika jamii ya Waamerika ni dhidi ya jamii ndogo ya watu wasio wazungu na wa dini za waliowachache hasa Waislamu.

Jioni ya Jumatatu, Mei 25, 2020, Floyd alikabiliwa na utumiaji mabavu na ukatili wa polisi mzungu mbaguzi wa rangi aliyemfunga pingu na kumlazimisha alale kifudifudi chini. Afisa huyu wa polisi alibana goti lake kwenye shingo ya Floyd na kusababisha kifo chake cha taratibu na cha kuhuzunisha. Wakati wote huo Floyed aliendelea kupiga kelele akisema, "Siwezi kupumua."

Mnamo Mei 29, baada ya kukamatwa, Chauvin alishtakiwa kwa mauaji ya daraja la tatu na kisha kuachiliwa kwa dhamana ya dola 500,000. Ingawa Chauvin alishtakiwa Machi 2021 kwa shtaka la mauaji ya daraja la pili na hatimaye kuhukumiwa kifungo cha miaka 23 jela, lakini kifungo hicho ambacho kwa hakika ni hafifu, hakikuzuia polisi wazungu wabaguzi  kuendelea kutumia mabavu dhidi ya Wamarekani wenye asili ya Afrika. 

Katika tukio la hivi punde kuhusiana na hilo, Jumamosi iliyopita asubuhi, kijana mwenye asili ya Afrika mwenye umri wa miaka 11 katika mji mdogo wa Indianola katika jimbo la Mississippi, ambaye aliwaita polisi kwa dharura kuingilia kati mzozo wa familia, alipigwa risasi na kujeruhiwa vibaya. Idara ya Polisi ya Mississippi inasema afisa aliyemfyatulia risasi mtoto huyo ameenda likizo ya lazima.

Mnamo Julai 2014, "Eric Garner", Mmarekani mwenye asilia ya Afrika, aliuawa na polisi wa Marekani huko New York kutokana na kubanwa shingo na kifua huku akisema "Siwezi kupumua". Katika miaka iliyopita, idadi kubwa ya watu weusi wamekufa kutokana na utumiaji mabavu wa polisi wa Marekani, na miongoni mwao tunaweza kuwataja Michael Brown, Walter Scott na Tamir Rice.

Mauaji ya kikatili ya George Floyd yaliyofanywa na Derek Chauvin yalitangazwa na vyombo vya habari na klipu zake kurushwa kwenye mitandao ya kijamii, na kusababisha maandamano makubwa ambayo hayajawahi kushuhudiwa kote Marekani kwa ajili ya kulaani ubaguzi wa rangi uliokita mizizi katika muundo wa jamii ya Marekani na unyanyasaji wa polisi dhidi ya watu weusi. Maandamano hayo yaliyoenea na ya nchi nzima na duniani kote ni maarufu kama vuguvugu la "Black Lives Matter" yaani 'Maisha ya Watu Weusi Ni Muhimu'.

Suala muhimu ni mbinu ya upendeleo na kwa kweli upuuzaji wa mfumo wa mahakama wa Marekani katika kuwashughulikia na kuwaadhibu wahusika wa unyanyasaji dhidi ya Wamarekani wenye asili ya Afrika. Tukiangazia vikao vya mahakama kuhusu kesi za maafisa wa polisi wazungu wanaowaua na kuwanyanyasa Wamarekani Waafrika tunaona kuna mtazamo wa kibaguzi katika mahakama wakati wa kushughulikia kesi hizo, jambo ambalo mara nyingi limesababisha polisi wauaji na makatili kuachiwa huru.

Mtaalamu wa masuala ya kijamii Justin Feldman asema: “Miongoni mwa nchi zilizoendelea, Marekani inaongoza kwa matukio ya polisi wanaowaua raia kiholela. Sio tu kwamba Marekani imeorodheshwa ya kwanza katika idadi ya watu waliouawa kutokana na utumiaji mabavu nje ya sheria unaotekelezwa na polisi, lakini pia polisi nchini humo hawawajibishwi kisheria au kisiasa kutokana na jina zao.

Kwa hivyo ilionekana wazi kwamba mahakama ya Marekani haikuwa na chaguo isipokuwa kutoa kifungo hafifu cha jela kwa Derek Chauvin aliyemuua kinyama George Floyd. Sasa, matakwa ya umma nchini Marekani, hasa kutoka kwa raia wenye asili ya Afrika ni utekelezaji wa haki na sera za kukomesha unyanyasaji na mauaji yaliyoratibiwa ya polisi wazungu wa Marekani dhidi ya watu wenye asili ya Afrika.

342/