Main Title

source : Parstoday
Jumapili

28 Mei 2023

19:54:00
1369420

Askari 2 wa Iran wauawa katika shambulio la kichokozi la Taliban; utulivu warejea

Askari wawili wa mpakani wa Iran wameuawa shahidi huku raia wawili wakijeruhiwa katika shambulizi la kichokozi la wapiganaji wa Taliban katika mpaka wa Jamhuri ya Kiislamu na Afghanistan.

Qassem Rezaei, Mkuu wa Jeshi la Polisi la Iran amesema vikosi vya Taliban hapo jana vilishambulia kwa kila aina ya silaha kituo cha polisi cha Sasoli katika mpaka wa Zabol.

Amesema askari shupavu wa Gadi ya Mpakani ya Iran walijibu uchokozi huo wa wapiganaji wa Taliban kutoka Afghanistan, na kutoa onyo kali dhidi ya kuchukuliwa hatua kama hiyo ya kichokozi.  

Mapigano yalizuka mapema jana kati ya Vikosi vya Walinzi wa Mpaka wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na vikosi vya Taliban kwenye mpaka wa Sistan na Baluchistan ya Iran na mkoa wa Nimroz wa Afghanistan, na katika maeneo mengine ya kandokando ya vijiji kadhaa ikiwa ni pamoja na Sasoli, Hatem na Makki.

Alireza Marhamati, Naibu Gavana wa mkoa wa Sistan na Baluchistan ya Iran amesema mapigano hayo yamemalizika na hali ya utulivu imerejea. Inaarifiwa kuwa, pande mbili zimeketi kuchunguza sababu zilizopelekea kutokea mikwaruzano hiyo.

Naye Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya serikali ya Taliban, Abdul Nafi Takor, amesema askari mmoja wa Gadi ya Mpakani ya Afghanistan ameuawa kwenye mapigano hayo katika mpaka wa Nimroz.

Mapigano hayo yamejiri siku chache baada ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran kusema kuwa Jamhuri ya Kiislamu haiutambua mfumo wa serikali unaoongoza hivi sasa nchini Afghanistan, sanjari na kusisitiza juu ya haja ya kuundwa serikali jumuishi katika nchi hiyo.

342/