Main Title

source : Parstoday
Alhamisi

10 Agosti 2023

15:22:16
1386161

Baada ya vita na wanamgambo waasi, jeshi la Ethiopia linadhibiti tena miji mikubwa ya Amhara

Serikali ya Ethiopia imetangaza kuwa imekomboa miji mikubwa katika eneo la Amhara kutoka kwa "magenge la wanamgambo waasi", baada ya siku kadhaa za vita kati ya jeshi la serikali kuu na wanamgambo wa eneo hilo.

Taarifa iliyotolewa na Mamlaka ya Dharura ya Serikali ya Shirikisho imesema, miji hiyo imekombolewa kutoka kwenye hatari ya magenge ya wanamgambo, ikiorodhesha miji 6, ikiwa ni pamoja na Bahir Dar, makao makuu ya eneo la Amhara, na "mji mtakatifu wa Lalibela".

Mwanachama wa wanamgambo wa Fano katika mji wa Gondar pia ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba vikosi vya ulinzi vya jeshi la Ethiopia, vikisaidiwa na polisi wa kutuliza ghasia na wanamgambo wanaoiunga mkono serikali, waliwafukuza wapiganaji wa Fano kutoka mji huo siku ya Jumanne.

Ameongeza kuwa: "Yalikuwa mapigano makali na kwamba Jeshi la Ulinzi la Taifa lilitumia vifaru huku wapiganaji waasi wakitumia bunduki za Kalashnikov pekee."

Afisa wa eneo la Gondar ameelezea kuwa, jeshi la Ethiopia sasa linadhibiti kikamilifu mji huo.

Wakati huo huo, Shirika la Ndege la Ethiopian Airlines limetangaza kuwa litaanzisha tena safari zake kuelekea Gondar na Bahir Dar, mji mkuu wa Amhara, leo Alkhamisi.

Awali madaktari wa Bahir Dar, makao makuu ya eneo la Amhara nchini Ethiopia, waliziambia duru za habari kwamba idadi kubwa ya raia wameuawa katika mapigano ya hivi majuzi kati ya wanamgambo wa eneo hilo na wanajeshi wa serikali.

Mapigano hayo yalizuka wiki iliyopita katika eneo la pili kwa ukubwa nchini Ethiopia kati ya wanamgambo wa Fano na Jeshi la Ulinzi la Ethiopia.

342/