Main Title

source : Parstoday
Jumapili

28 Januari 2024

17:49:40
1433246

Iran yatuma angani satalaiti tatu kwa mafanikio

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imefanikiwa kutuma angani satalaiti tatu kwa mpigo zilizotengenezwa na wataalamu wa hapa nchini.

Kwa mujibu wa shirika la habari la IRNA, satalaiti hizo za Mahda, Keyhan-2, na Hatef-1 zimetumwa angani mapema leo Jumapili kwa kutumia roketi la  kubeba satalaiti la Simorgh.

Satalaiti hizo za utafiti zilizotengenezwa na Kituo cha Utafiti wa Anga za Juu cha Iran zimewekwa kwa mafanikio katika mzingo uliokusudiwa, umbali wa kilomita baina ya 450 na 1,100 juu ya uso wa dunia.

Haya yanajiri siku chache baada ya satalaiti ya Thuraya ambayo imebuniwa na kutengenezwa kwa juhudi na hima ya wasomi vijana wa Iran na kurushwa katika anga za juu, kufanikiwa kutuma taarifa zake za awali na kuthibitisha kuwa imetua sehemu iliyokusudiwa kwa mafanikio makubwa.

Nafasi ya Iran katika sekta ya utaalamu wa anga za mbali imeimarika sana kwenye miaka ya hivi karibuni. Iran imeweza kubuni na kutengeneza satalaiti za kila namna za kielimu, kiutafiti, kijiografia na kijeshi. Mafanikio hayo yote yamepatikana pamoja na kuwa nchi hii imewekewa vikwazo na madola ya Magharibi yakiongozwa na Marekani.

Wakati huo huo, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, jana Jumamosi alilaani vikali taarifa ya "uingiliaji kati" ya serikali za Uingereza, Ujerumani na Ufaransa kuhusu kurushwa angani satalaiti mpya ya Thuraya iliyoundwa na vijana wa taifa hili.

Nasser Kan'ani amesisitiza kuwa, maendeleo ya kisayansi na utafiti, ikiwa ni pamoja na katika masuala ya anga na anga za mbali, ni haki ya wazi na isiyopingika ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

342/