Main Title

source : Parstoday
Ijumaa

19 Aprili 2024

18:31:26
1452477

Wizara ya Ulinzi: Magaidi 9 wa al-Shabaab wameangamizwa katika operesheni ya kijeshi Somalia

Wizara ya Ulinzi ya Somalia imetangaza habari ya kuangamizwa magaidi tisa wa al-Shabaab katika eneo la Bay la kusini mwa nchi hiyo ya eneo la Pembe ya Afrika.

Sehemu moja ya taarifa hiyo imesema: "Jeshi la Taifa la Somalia limefanikiwa kuvamia kambi ya al-Shabaab katika kijiji cha Taflow."

Sehemu nyingine ya taarifa hiyo imesema: "Oporesheni ya Jeshi la Taifa imesambaratisha kambi hiyo, kuangamiza magaidi 9 na kukamata akiba ya silaha na masanduku ya risasi."

Somalia imekuwa ikikabiliwa na ukosefu wa usalama kwa miaka mingi, huku vitisho vikuu vikitoka kwa genge la kigaidi la al-Shabaab na makundi mengine ya kigaidi kama vile Daesh au ISIS.

Tangu mwaka 2007, magaidi wa al-Shabaab wamekuwa wakipigana na serikali ya Somalia na Kikosi cha Umoja wa Afrika nchini humo (ATMIS) lakini mashambulizi yake yamekuwa yakifeli hasa baada ya genge hilo kufurushwa kwenye miji mikubwa ya Somalia na kubakia katika baadhi ya vijiji ambako inavitumia kuendesha mashambulizi ya kuvizia na ya chini kwa chini. 

Kikosi cha ATMIS cha Umoja wa Afrika kimetumwa huko Somalia kwa baraka kamili za  Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Genge la kigaidi la al-Shabab limeongeza mashambulizi yake tangu Rais wa Somalia, Hassan Sheikh Mohamud kutangaza "vita vya kila namna" dhidi ya genge hilo kampeni ambayo inaonekana imefanikiwa kiasi kwamba hivi sasa kikosi cha ATMIS cha Umoja wa Afrika kimeshaanza mchakato wa kuondoa askari wake nchini humo ili kukabidhi masuala yote ya ulinzi kwa vikosi vya serikali ya Somalia.

342/