Main Title

source : Parstoday
Jumatano

29 Mei 2024

20:58:01
1462137

Licha ya mauaji ya Rafah, US yasema Israel bado haijavuka 'mstari mwekundu' wa Biden

Msemaji wa Baraza la Usalama wa Taifa la Marekani John Kirby amedai kuwa Israel haijakiuka "mstari mwekundu" wa Rais Joe Biden wa kuifanya Washington isitishe katika siku za usoni kuipatia Tel Aviv silaha za mashambulizi kwa sababu inavyohisi Marekani Israel haitaanzisha operesheni ya ardhini ya kuuvamia kikamilifu mji wa Rafah wa kusini mwa Ukanda wa Ghaza.

Licha ya kutoa kauli ya kulaani mauaji ya halaiki yaliyofanywa na utawala wa Kizayuni mwishoni mwa wiki katika kambi ya wakimbizi mjini Rafah yaliyopelekea Wapalestina wapatao 50 kuuawa shahidi na 250 kujeruhiwa, na kuyaelezea mauaji hayo kuwa ni  "ya kusonensha moyo" na "ya kutisha", lakini Kirby amesema Marekani haipangi kufanya mabadiliko yoyote katika sera zake kutokana na vitendo vya Israel.

Ameongeza kuwa Marekani inafuatilia matokeo ya uchunguzi unaofanywa na Israel yenyewe kuhusu kile ambacho serikali ya utawala huo wa Kizayuni imekiita kuwa ni "shambulio lililofanywa kwa usahihi".

Hayo yanajiri huku utawala wa Kizayuni ukiendelea kubadilisha kila baada ya muda maelezo ya 'simulizi' yake kuhusiana na kilichojiri hasa katika shambulio la Jumapili usiku katika kambi ya wakimbizi Wapalestina mjini Rafah kusini mwa Ghaza.

Hapo awali, vikosi vya jeshi la Kizayuni vilisema vilifanya "mashambulizi yenye usahihi" kwa kutumia "silaha zinazolenga kwa usahihi" kuwalenga wanachama wa Hamas huko Rafah ambako Wapalestina waliolazimika kuhama makazi yao walikuwa wametafuta hifadhi. Lakini baada ya shambulio la kinyama kulaaniwa vikali kimataifa, waziri mkuu mshupalia vita wa Israel  Benjamin Netanyahu aliliita shambulio la Rafah kuwa ni "kosa la kimaafa." Na hivi sasa utawala haramu wa Kizayuni unadai kuwa mauaji hayo ya raia Wapalestina yalitokana na mripuko wa pili uliotokea baada ya shambulio lake lililolenga wapiganaji wawili wa Hamas.

Picha na video zinazoonyesha viwiliwili vilivyokatika katika na kuteketea kwa moto, baadhi yao vikiwa ni vya watoto wachanga, zimeibua vilio na hisia kali za kimataifa na kuwafanya makumi ya maelfu ya watu waingie barabarani na kuandamana katika miji ya nchi za Magharibi kulaani jinai hiyo ya Israel.../

342/