Uchaguzi wa leo unafanyika baada ya kutopatikana mgombea aliyepata zaidi ya asilimia 50 ya kura katika uchaguzi wa raundi ya kwanza uliofanyiika Ijumaa iliyopita baina ya wagombea wanne waliochuana katika awamu hiyo.
Veterani wa vita vya Saddam Hussein dhidi ya Iran, Saeed Jalili, ambaye aliwahi kuwa Mkuu wa Baraza la Usalama wa Taifa na kiongozi wa timu ya Iran katika mazungumzo ya nyuklia na nchi za Magharibi, anachuana na waziri wa zamani wa afya, Daktari Masoud Pezeshkian. Wawili hawa walipata kura nyingi zaidi katika duru ya kwanza ya uchaguzi wa rais wa Iran Ijumaa iliyopita.Wairani wasiopungua milioni 61 walitimiza masharti ya kupiga kura. Awali, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu alieleza umuhimu wa kushiriki kwa wingi wananchi katika duru ya pili ya uchaguzi wa Rais wa Iran na kusisitiza kuwa, kadiri ushiriki wa wananchi unavyokuwa mkubwa ndivyo serikali pia itakavyoweza kutimiza malengo yake ndani ya nchi na kufuatilia malengo mbalimbali katika kalibu ya mkakati mkuu wa nchi. Ayatullah Ali Khamenei amesema kwamba, uchaguzi huu ni muhimu sana na kwamba kila mtu anayeunga mkono Uislamu, Jamhuri ya Kiislamu, maendeleo na ustawi wa nchi na suala la kuondoa mapungufu yaliyopo, anaweza kuonyesha uungaji mkono huo siku ya Ijumaa kwa kushiriki katika uchaguzi. Kaimu Rais wa Jamhuri ya Kiislamu, Mohammad Mokhbar pia amewahimiza wananchi kushiriki kwa wingi katika uchaguzi wa urais wa leo na kuwa na nafasi athirifu katika kuamua hatima yao na ya nchi yao.
342/