Masoud Pezeshkian aliyasema hayo siku ya Jumatano katika barua yake kwa Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas), Ismail Haniyeh.
Katika barua yake hiyo, Pezeshkian ametoa shukrani zake za dhati kwa ujumbe wa pongezi wa Ismail Haniyeh kufuatia ushindi wake katika uchaguzi wa rais wa Iran.Masoud Pezeshkian amesema katika barua hiyo kwamba kwa mujibu wa malengo matukufu ya Mapinduzi ya Kiislamu, fikra za Imam Khomeini (MA) na miongozo ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran Ayatullah Ali Khamenei, Iran inauchukulia kuwa wajibu wake wa kibinadamu na wa Kiislamu, kuliunga mkono taifa madhlumu la Palestina na mapambano yake dhidi ya uvamizi na ubaguzi wa rangi unaofanywa na utawala wa Kizayuni.
Amesema, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itaendelea kuliunga mkono taifa linalodhulumiwa la Palestina hadi kufikiwa malengo na haki zake zote na vile vile kukombolewa Quds tukufu.
Masoud Pezeshkian, Rais mteule wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa, kwa kuzingatia uimara wa kihistoria wa taifa la Palestina na ushujaa wa wapiganaji wa muqawama katika kukabiliana na Wazayuni, bila shaka ushindi wa mwisho utakuwa wa "Palestina pendwa".
342/