17 Julai 2024 - 19:04
Sisitizo la Iran juu ya Umoja wa Mataifa kutoruhusu hatua za mabavu za upande mmoja

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran anayeshughulikia masuala ya kisheria na kimataifa amesema, Umoja wa Mataifa unapaswa kupinga wazi hatua za mabavu na za upande mmoja zinazotekelezwa na baadhi ya madola yenye kiburi duniani, na kuyataka yakomeshe hatua hizo mara moja.

Katika miongo ya hivi karibuni, vikwazo vya aina mbalimbali vimekuwa vikitumiwa na nchi za kibeberu kama chombo cha kuzishinikiza nchi huru zinazojitawala duniani. Tangu mwanzoni mwa miaka ya 1990, Marekani, Umoja wa Ulaya na mataifa mengine yenye uchumi ulioendelea yameweka mamia ya vikwazo vya kiuchumi dhidi ya nchi nyingine.

Akizungumza karibuni katika kikao cha Baraza Kuu la Kisiasa la Umoja wa Mataifa mjini New York, Reza Najafi, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran anayeshughulikia masuala ya kisheria na kimataifa ameongeza kwamba, hatua za mabavu na za upande mmoja (UCMs) ni kikwazo kikubwa kwa ushirikiano wa kimataifa na bila shaka zinadhoofisha shughuli za mfumo wa Umoja wa Mataifa na kuvuruga maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya nchi zinazoendelea. Amesema hatua hizo zinavuruga juhudi za kuimarisha ushirikiano wa pande kadhaa na kuimarisha misimamo ya upande mmoja.

Huku akisisitiza kuwa suala la maendeleo ya nchi linapaswa kuwa kitovu cha umakini na juhudi za Umoja wa Mataifa na ushirikiano wa kimataifa, Najafi amesisitiza umuhimu wa nchi zilizoendelea kutekeleza ahadi zao katika kudhamini mahitaji ya kifedha, uhamishaji wa teknolojia na uwezeshaji na kuongeza kuwa Umoja wa Mataifa unapasa kutekeleza jukumu lake la msingi ambalo ni kuimarisha ushirikiano wa kimataifa.

Naibu Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran amefafanua maendeleo makubwa iliyoyafikia Iran katika fremu ya uchumi wa muqawama hususan katika uga wa kupunguza umaskini, kuimarisha na kueneza uadilifu wa kijamii, kuhakikisha usalama wa chakula, kuwawezesha wanawake na wasichana, kuimarisha teknolojia na uvumbuzi na kulinda mazingira.

Kwa zaidi ya miongo 4 sasa, tangu ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, maadui wa wananchi wa Iran daima wamekuwa wakijaribu kuyumbisha na kuvuruga uchumi wa Iran kwa kutekeleza vikwazo vya kidhalimu visivyo na mwisho dhidi ya taifa hili la Kiislamu.

342/