26 Julai 2024 - 17:09
Iran yakaribisha makubaliano ya kurejeshwa safari za ndege mjini Sana'a, Yemen

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amekaribisha taarifa ya mwakilishi maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Yemen kuhusiana na makubaliano yaliyofikiwa ya kurejeshwa safari za ndege katika uwanja wa ndege wa Sana'a mji mkuu wa Yemen na kutatuliwa matatizo ya fedha na kibenki kote nchini humo.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Fars, Hans Grundberg, mwakilishi maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Yemen ametoa taarifa kuhusu kufikiwa makubaliano ya kurejeshwa safari za ndege katika uwanja wa ndege wa Sana'a na kutatuliwa matatizo ya fedha na benki kote nchini humo.

Nasser Kan'ani, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran alisema jana Alhamisi kuwa, Tehran imepokea vizuri uamuzi huo.

Mohammad Abdul Salaam msemaji wa timu ya mazungumzo ya Serikali ya Wokovu wa Kitaifa ya Yemen yenye makao makuu yake mjini San'a amesema kuwa, makubaliano yao hayo na Saudi Arabia yana vifungu vinne. 

Nasser Kan'ani amekaribisha makubaliano yaliyofikiwa baina ya pande hizo mbili na kusema: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inakaribisha kwa mikono miwili makubaliano yoyote ambayo yatapunguza mashinikizo ya kiuchumi, yataharakisha kuondolewa vikwazo, yatawanufaisha wananchi na kuleta utulivu na amani katika eneo hili. 

Aidha Msemaji huyo wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameashiria sera ya kimsingi ya Jamhuri ya Kiislamu ya kupigania kutatuliwa migogoro ya kieneo kwa njia ya mazungumzo na kusema kwamba, anatumai kuona kunatiwa saini makubaliano ya amani ya kudumu nchini Yemen haraka iwezekanavyo. 

342/