Sisitizo hilo limetolewa na Abdullatif bin Rashid al-Zayani, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Bahrain katika mazungumzo yake kwa njia ya simu na mwenzake wa Iran Sayyid Abbas Araghchi.
Katika mazungumzo hayo ya simu, Abdullatif bin Rashid Al Zayani Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Bahrain amempongeza Abbas Araghchi kwa kuteuliwa kuwa Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran na kumtakia mafanikio mema katika nafasi yake mpya.
Akiangazia umuhimu wa uhusiano wa pande mbili na Iran, Al Zayani ameelezea matumaini kwamba kipindi hiki kipya kitakuza mazungumzo ya pamoja ya kisiasa kati ya Tehran na Manama.
Kwa upande wake Abbas Araghchi, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran amemshukuru mwenzake wa Bahrain kwa pongezi zake, pamoja na kuhudhuria sherehe za kuapishwa Rais Masoud Pezeshkian.
Aidha amesema, kustawisha uhusiano na nchi jirani ni sehemu ya sera ya ujirani ya Iran.
Bahrain iliifuata Saudi Arabia kuvunja uhusiano wa kidiplomasia na Iran mnamo Januari 4, 2016, baada ya waandamanaji nchini Iran walioghadhibishwa na kunyongwa mwanazuoni mashuhuri wa madhehebu ya Shia Sheikh Nimr Baqir al-Nimr na serikali ya Saudia kuvamia jengo la ubalozi wa nchi hiyo hapa mjini Tehran.
Juni mwaka huu Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Bahrain zilitoa taarifa ya pamoja zikielezea kuwekwa mikakati muhimu ya kuanzisha mazungumzo baina ya nchi mbili kwa lengo la kuchunguza namna ya kurejesha uhusiano wa kisiasa.
342/