Khalil al-Hiyya amesema: Makubaliano yoyote yanapaswa kujumuisha kusitisha uchokozi kikamilifu, kuondoa askari vamizi eneo la Gaza, ikiwa ni pamoja na mhimili wa Philadelphia, uhuru wa wakimbizi kurejea kwenye makazi yao, na kusaidia ujenzi mpya wa maeneo yaliyoharibiwa na utawala wa Kizayuni wa Israel. Khalil Al-Hiyya ameongeza kuwa: "Ulimwengu unajua ni nani anayekwamisha makubaliano ya kusitisha vita ambaye anatoa visingizio vya mara kwa mara vya kukwamisha juhudi za kufikia muafaka. Na haya ndivyo yaliyothibitishwa na Rais wa Marekani, Joe Biden, kuwa Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, hafanyi juhudi za kutosha za kukamilisha makubaliano ya kusimamisha mapigano."
Maafisa wa utawala wa Kizayuni wa Israel pia daima wamekuwa wakikiri kwamba, Netanyahu anaendelea kudanganya na kusema uongo katika mchakato wa mazungumzo ya kusitisha vita vya Gaza. Mazungumzo hayo yamefanyika katika awamu kadhaa huko Cairo na Doha, lakini kila mara utawala wa Kizayuni umekuwa ukikwamisha kufikiwa makubaliano kwa kutoa matakwa yasiyo na msingi na madai ya uongo.
Hamas na makundi ya Muqawama ya Palestina pia yamesisitiza kuwa, yako tayari kuendelea na mazungumzo kwa sharti la kutekelezwa matakwa halali ya watu wa Palestina na kukabiliana na sera za uvamizi za utawala wa Kizayuni wa Israel. Vikwao vinavyowekwa na Netanyahu, akisaidiwa na serikali ya Marekani ikiwa ndio muungaji mkono mkuu wa utawala wa Kizayuni, pia ni moja ya sababu kuu za kufeli mazungumzo ya usitishaji vita katika miezi ya hivi karibuni.
Nadav Argaman, mkuu wa zamani wa Shirika la Ujasusi na Usalama wa Ndani wa Israel (Shin Bet), amekiri kuwa "Benjamin Netanyahu ni mtu dhalimu, asiye na matumaini na mlaghai ambaye anajaribu kuipotosha nchi nzima kwa uongo wa Philadelphia ili kuzuia makubaliano ya kusitisha vita". Argaman anasema: "Netanyahu ametoa kafara maisha ya mateka wa vita na usalama wa Israel kwa ajili ya maslahi yake binafsi na kwa ajili ya muungano wake wa (Wazayuni wenye misimamo mikali)."
Mhimili wa Philadelphia ni ukanda mwembamba wa mpaka wenye urefu wa kilomita 14 na upana wa kati ya mita 100 na 300, ambao uko kwenye mpaka kati ya Gaza na Misri. Eneo hili lilianzishwa kama ukanda wa kutenganisha Gaza na Misri, na ni muhimu sana kwa mtazamo wa kiusalama na kijeshi. Jeshi la utawala wa Kizayuni limeharibu kivitendo uwezekano wa kuwepo usitishaji vita kwa kuvamia na kukalia kwa mabavu mhimili wa Philadelphia, na nchi za Qatar, Misri na Marekani, zinazopatanisha katika mazungumzo hayo, zinataka jeshi la Israel liondolewe katika eneo hilo. Kwa miaka mingi, eneo hilo limepewa mazingatio makubwa kwa sababu ya njia za chini ya ardhi zinazounganisha Gaza na Misri. Njia hizo ziliruhusu makundi mbalimbali ya Wapalestina kutuma vifaa mbalimbali, ikiwa ni pamoja na chakula, dawa, silaha, mafuta na bidhaa nyingine katika eneo la Gaza.
Sisitizo la Netanyahu la kuendelea kulikalia kwa mabavu eneo la Ukanda wa Gaza na kuendelea kuwepo wanajeshi wa Israel katika mhimili wa Philadelphia ndiyo sababu kuu za kutofikiwa makubaliano katika mazungumzo ya kuhitimisha vita. Kuendelea kulikaliwa kwa mabavu eneo la Philadelphia ni kinyume na sheria na kanuni za kimataifa, na utawala wa Kizayuni wa Israel unang'ang'ania msimamo wake wa kuendelea kulikalia eneo hilo kwa uungaji mkono wa White House.
Vyovyote iwavyo, Hamas inasisitiza masuala mawili muhimu na ya kimsingi katika mazungumzo ya usitishaji vita ambayo ni kuondoka majeshi ya Israel huko Gaza na dhamana ya kurejea wakimbizi wa Kipalestina katika maeneo yao. Hata hivyo, utawala wa Kizayuni wa Israel na washirika wake wanakwamisha mazungumzo ya usitishaji vita kwa kutekeleza hatua zinazokinzana na sheria za kimataifa na kuendelea kufanya jinai za kivita na mauaji ya kimbari dhidi ya raia wa Palestina katika Ukanda wa Gaza.
342/