Nabih Beri Spika wa bunge la Lebanon amesisitiza kuwa Benjamin Netanyahu Waziri Mkuu wa Israel anaendeleza hatua zake za kuligeuza eneo la kusini mwa Lebanon kuwa ardhi iliyoungua ambayo haifai kuishi yoyote kwa kutumia mabomu ya fosforasi kuharibu ardhi ya kijani kibichi ya kilimo.
Spika wa bunge la Lebanon pia ameashiria hujuma za Israel za kushambulia nyumba za raia wa Lebanon na kuwauwa khususan wanawake, watoto na wazee, wafanyakazi wa huduma za misaada na wa sekta ya afya nchini humo.
Nabih Berri amesema Lebanon haitaki vita lakini ina haki ya kujilinda kwa nguvu zote na kwamba haitaacha kufanya jitihada ili kuizuia Israel kuwahamisha wakazi wa maeneo ya kusini mwa nchi hiyo.
Spika wa bunge la Lebanon ameitolea wito jamii ya kimataifa iishinikize Israel na kuulazimisha utawala huo kusitisha hujuma zake dhidi ya nchi hiyo.
Ijumaa tarehe 20 Septemba jeshi la Israel lilishambulia eneo la Dhahiya kusini mwa mji mkuu wa Lebanon, Beirut na kulenga jengo moja, hujuma ambayo ilipelekea kuuawa shahidi raia 45 wa Lebanon, akiwemo Ibrahim Aqeel, mmoja wa makamanda wa harakati ya muqawama ya Hizbollah na makumi ya maelfu kujeruhiwa.
Wakati huo huo, Ndege za kivita za utawala ghasibu wa Israel zimefanya mashambulizi makali dhidi ya miji na vijiji vya Lebanon na kuua takriban watu 274.
Wizara ya afya ya nchi hiyo ilitangaza idadi ya vifo siku ya Jumatatu, ikisema "zaidi ya 1000" wengine pia wamejeruhiwa katika mashambulizi yaliyolenga maeneo kadhaa.
Waliojeruhiwa au kuuawa ni pamoja na "watoto, wanawake, na wafanyikazi wa dharura," huku ikitabiriwa kuwa idadi hiyo yaweza kuongezeka.
Vyombo vya habari vya Lebanon vimetangaza ndege za kivita za utawala dhalimu wa Israel zilishambulia kwa mabomu miji na vijiji vyote vilivyo kwenye mpaka wa kusini.
Ndege za kivita za Israel pia zimeripotiwa kulenga maeneo ya mashariki mwa Lebanon, likiwemo Bonde la Bekaa.
Duru za Lebanon zimesema mashambulizi hayo ya anga yalilenga jumla ya maeneo zaidi ya 40 nchini Lebanon .
Wakati huo huo, Najib Mikati, kaimu waziri mkuu wa Lebanon amezungumza Jumatatu katika mkutano wa baraza la mawaziri na kusema: "Kupanuka kwa uchokozi wa Israel dhidi ya Lebanon ni mauaji ya kimbari kwa kila maana ya neno, lengo likiwa ni kuangamiza vijiji vya Lebanon."