Main Title

source : Pars Today
Jumatatu

16 Septemba 2019

08:14:38
975882

Ukosoaji mkali wa Harakati ya HAMAS dhidi ya Saudi Arabia

Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS imetoa taarifa, ambayo kwa mara nyingine tena imeikosoa vikali Saudi Arabia na kuwataka viongozi wa nchi hiyo wamuachilie huru mmoja wa viongozi wandamizi wa harakati hiyo anayeshikiliwa nchini humo.

(ABNA24.com) Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS imetoa taarifa, ambayo kwa mara nyingine tena imeikosoa vikali Saudi Arabia na kuwataka viongozi wa nchi hiyo wamuachilie huru mmoja wa viongozi wandamizi wa harakati hiyo anayeshikiliwa nchini humo.

Tarehe nne Aprili mwaka huu, vyombo vya usalama vya Saudia vilimtia mbaroni Muḥammad al-Khidhri, mmoja wa viongozi wandamizi wa harakati ya HAMAS mjini Jeddah ambaye alikuwa akiishi katika mji huo kwa karibu miongo mitatu. Gazeti la Lebanon la al-Akhbar limeandika kuwa, idadi ya viongozi wa harakati ya HAMAS wanaoshikiliwa nchini Saudia ni zaidi ya 60. Ilipomtia mbaroni Muḥammad al-Khidhri, serikali ya Saudia haikutaja sababu yoyote ya kuchukua hatua hiyo, hata hivyo harakati hiyo ya muqawama imetangaza kuwa, kiongozi wake huyo hakuwa akifanya lolote nchini Saudia ghairi ya kukusanya misaada ya kifedha tu kwa ajili ya mateka wa Kipalestina wanaozuiliwa katika jela za kutisha za utawala haramu wa Israel. Suala lingine ni hili kwamba Muḥammad al-Khidhri na viongozi wengine waandamizi wa harakati ya HAMAS ambao wanazuiliwa katika jela za Saudia, wanapitia wakati mgumu kutokana na kuteswa na maafisa usalama wa nchi hiyo. Mmoja wa viongozi wa harakati hiyo ya Kiislamu ameuambia mtandao wa habari wa Arabi 21, kwamba, mateka hao wana hali mbaya, huku serikali ya Saudia ikiwa imewafungia akaunti zao za fedha, na kwamba familia zao pia zina hali mbaya ya kimaisha. Mienendo hiyo ya Saudi Arabia ya kuwaandama viongozi na wanachama wa harakati ya HAMAS, inadhihirisha wazi kuwa, utawala wa Aal Saud hauna uhusiano mzuri na harakati hiyo.

Hii ni katika hali ambayo kwa mtazamo wa kikaumu, harakati ya HAMAS ni ya Kiarabu, na kwa mtazamo wa kidini, ni harakati ya Kiislamu na ya madhehebi ya Suni. Kwa msingi huo, kwa mtazamo wa kikaumu na kidini, hakuna mgongano wowote kati ya Saudia na harakati ya Hamas. Kile ambacho kimepelekea kuwepo na mgongano na hata uhasama katika uhusiano wa Saudia na harakati hiyo ya Kiislamu, ni tofauti za utambulisho wa kisiasa kati ya pande mbili hizo. Hii ni kusema kuwa, harakati hiyo ni moja ya makundi ya mrengo wa muqawama ambayo yamekuwa yakipinga aina yoyote ya maridhiano na mapatano na utawala haramu wa Kizayuni wa Israel, kama ambavyo pia inapinga uingiliaji wa madola yaliyo nje ya eneo katika masuala ya eneo la Asia Magharibi. Na hii ni katika hali ambayo Saudia, hususan baada ya kuingia madarakani Mfalme Salman bin Abdulaziz Al Saud na mtoto wake, Mohammad Bin Salman, imekuwa na msimamo mkali dhidi ya muqawama, ikiwemo kuchukua hatua kali dhidi ya harakati ya muqawama wa Kiislamu ya Palestina (HAMAS). Katika uwanja huo, utawala wa Aal-Saud unasema, harakati hiyo ina misimamo ya kufurutu ada. Ama nukta nyingine ni kwamba, kwa kuzingatia mgongano wa utambulisho wa kisiasa uliopo kati ya Saudia na HAMAS, kabla ya hapo pia ilikuwa ikitokea mivutano katika mahusiano ya pande mbili.

Hata hivyo mivutano hiyo ilikuwa ikimalizwa kupitia upatanishi wa pande maalumu. Katika mzozo wa sasa harakati ya HAMAS imejitahidi kuutatua kwa kutumia upatanishi wa upande wa tatu, hata hivyo Saudia chini ya uongozi wa Mfalme Salman bin Abdulaziz Al Saud, inaitazama harakati hiyo kama inavyozitazama nchi nyingine za Kiarabu, yaani mtazamo wa dharau, wa kutaka itiiwe na wadau wote wa Kiarabu. Katika uwanja huo HAMAS imetangaza kwamba, kwa kipindi cha miezi mitano na nusu iliyopita, imefanya juhudi kubwa kupitia upatanishi kwa lengo la kuhakikisha Muḥammad al-Khidhri mwenye umri wa miaka 81 anaachiwa huru, hata hivyo baada ya kuona juhudi na upatanishi huo haujawa na faida yoyote ndipo ikalazimika kulitangaza na kuliweka wazi suala hilo kwenye vyombo vya habari. Ama nukta ya mwisho ni hii kwamba utawala wa Aal Saud unajitapa kuwa muungaji mkono wa Palestina, katika hali ambayo madai na mienendo yake hii ikiwemo kuwatia mbaroni viongozi wa harakati ya HAMAS kwa upande mmoja, na pia siasa zake ghalati kama vile kuboresha uhusiano wake na utawala wa Kizayuni kwa upande wa pili, haviendani na madai yake hayo. Katika uwanja huo, Osama Hamdan kiongozi wa mahusiano ya kigeni wa harakati ya HAMAS, sambamba na kukosoa kitendo cha kuwatia mbaroni wajumbe na viongozi wa harakati hiyo kunakofanywa na Saudia, amesema: "Mtu ambaye anaifanyia kazi Palestina anatakiwa akirimiwe, na sio awe jela."




/129