(ABNA24.com) Baada ya kupita karibu mwaka mmoja tangu mauaji ya mwandishi na mkosoaji wa utawala wa Saudi Arabia Jamal Khashoggi, mrithi wa ufalme wa nchi hiyo Muhammad bin Salman amekana kuhusika na mauaji hayo lakini amekubali kubea dhima na lawama zake.
Bin Salman amesema katika mahojiano yake na televisheni ya PBS ya Marekani kwamba, anabeba lawama za mauaji ya Jamal Khashoggi kwa sababu yalifanyika wakati alipokuwa akisimamia masuala ya nchi. Wakati huo huo Bin Salman amesisitiza kuwa, hakuwa na habari kuhusu mauaji hayo.
Jamal Khashogi mwandishi wa gazeti la Washington Post tarehe Pili Oktoba 2018 alieleka katika ubalozi wa Saudia mjini Istanbul huko Uturuki kwa ajili ya masuala ya kiidara lakini kamwe hakutoka hai ubalozini humo. Timu ya askari usalama wa Saudi Araba iliyokuwa imetumwa Istanbul kwa kutumia ndege makhsusi ilimuua Jamal Khashoggi ndani ya ubalozi huo na maiti yake ikakatwa vipande vipande.
Serikali ya Saudi Arabia imekuwa ikitumia mbinu nne tofauti kuhusiana na mauaji ya Khashoggi. Kwanza ni kukana kabisa kuhusika kwa njia yoyote na mauaji hayo ya kutisha. Pili ni kukiri kwamba, jinai hiyo ilifanywa na askari usalama wa Saudia lakini maafisa rasmi wa serikali akiwemo mrithi wa ufalme Muhammad bin Salman hawakuhusika na jinai hiyo. Mbinu hii ya pili ilianza kutumiwa baada ya kushadidi mashinikizo ya kimataifa dhidi ya utawala wa Aal Saud. Mbinu ya tatu ni kuanzisha mahakama ya kimaonyesho ya kesi ya mauaji ya Khashoggi na kutoa hukumu ya kifo dhidi ya baadhi ya maafisa waliopewa amri ya kufanya mauaji hayo. Na mbinu ya nne ni hii ya Muhammad bin Salman kukubali kwa mara ya kwanza kabisa kubeba dhima na lawama za mauaji ya kinyama ya Jamal Khashoggi sambamba na kukana kwamba, alihusika na mauaji hayo.
Hapa linajitokeza swali muhimu kwamba, ni kwa nini Muhammad bin Salman ambaye katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita amekuwa akikanusha kuhusika kwa njia yoyote na mauaji ya Khashoggi amejitokeza hadharani na kukubali kubeba dhima na lawama za mauaji hayo?
Inaonekana kuwa, sababu kuu ya hatua hiyo ya Bin Salman ni kwamba nyaraka na ushahidi wote unathibitisha kuwa utawala wa Saudi Arabia ulihusika kikamilifu katika mauaji hayo ya kutisha na kwa msingi huo Bin Salman hawezi kukanusha uhakika huo.
Maudhui nyingine ni kwamba, kimsingi hakuna jipya katika hatua na matamshi ya sasa ya Muhammad bin Salman kwa sababu serikali ya Saudia ilikanusha kuhusika na mauaji hayo sambamba na kukubali kwa njia isiyo ya moja kwa moja kubeba dhima na lawama zake. Hivyo Muhammad bin Salman sambamba na kukana tena kwamba alihusika na mauaji hayo amekubali rasmi kubeba lawama zake, suala ambalo halitakuwa na gharama kwa utawala wa kiukoo wa Saudia ghairi ya kulipa hasara za kimaada tu. Vilevile hatua hiyo, kwa dhana ya Bin Salman, itamdhihirisha mtawala huyo kama mtu anayewajibika. Ni vyema kukumbusha hapa kuwa, Muhammad bin Salman anahitaji kusafisha sura yake na kujidhihirisha kama kiongozi mwema na mwenye misimamo ya wastani kwa ajili ya kuweza kukalia kiti cha ufalme wa Saudi Arabia.
Nukta nyingine ya kuashiriwa ni kwamba, kwa hatua yake hiyo Bin Salman ametaka kuwaambia walimwengu kwamba, nchini Saudia kama ilivyo katika nchi nyingine, yumkini likatokea jambo ambalo viongozi wake hawakuhusika nalo. Kwa maneno mengine ni kuwa, baada ya kupita mwaka mmoja sasa tangu mauaji ya kutisha ya Khashoggi, mrithi wa ufalme wa Saudia amekana tena kuhusika yeye na utawala wa baba yake na mauaji ya Khashoggi.
Pamoja na hayo yote matamshi hayo ya Bin Salman hayawezi kusafisha mikono yake iliyojaa damu ya Jamal Khashoggi. Hasa baada ya ripota maalumu wa Umoja wa Mataifa Agnès Callamard kutangaza kwamba, kumepatikana nyaraka na ushahidi madhubuti unaothibitisha kwamba maafisa wa ngazi za juu wa Saudi Arabia akiwemo Muhammad bin Salman walihusika na mauaji ya mwandishi na mkosoaji mkubwa wa utawala wa nchi hiyo, Jamal Khashoggi. Kabla ya hapo pia vyombo vya upelelezi vya Uturuki na shirika la ujasusi la Marekani CIA vilikuwa tayari vimethibitisha kwamba, Saudi Arabia na hasa Muhammad bin Salman mwenyewe alihusika moja kwa moja katika mauaji ya kutisha ya Jamal Khashoggi.
/129