19 Machi 2021 - 17:45
Samia Suluhu Hassan, sasa rasmi Rais wa 6 wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mama Samia Suluhu Hassan mapema leo asubuhi, saa nne asubuhi kwa majira ya Afrika Mashariki ameapishwa kuwa rais wa 6 wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika hafla ndogo iliyofanyika katika Ikulu ya Magogoni jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na marais wastaafu wa Tanzania na Zanzibar pamoja na viongozi wengine mbalimbali wa nchi hiyo.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Mara baada ya kuapishwa Rais Samia Suluhu Hassan amepigiwa mizinga 21 na kukagua gwaride maalumu kwa mara ya kwanza akiwa amirijeshi mkuu wa majeshi ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania.

Mama Samia amekuwa rais wa kwanza mwanamke kuwahi kutawala nchi za Afrika Mashariki. Vile vile ni rais wa kwanza mwanamke Muislamu kuwahi kutawala barani Afrika. 

Katika hotuba yake ya kwanza akiwa Rais wa Tanzania, Rais Samia Suluhu Hassan ametoa mwito wa umoja na mshikamano kwa Watanzania wote.

Kabla ya hapo, mkurugenzi msaidizi wa kitengo cha habari Maelezo Tanzania, Rodney Thadeus alikuwa amesema kuwa hafla ya uapisho itafanyika Ikulu Dar es Salaam saa 4 asubuhi na kushuhudiwa Samia akiwa rais wa sita wa Tanzania kuchukua nafasi ya Dk John Magufuli aliyefariki dunia  Machi 17,  2021.

Jana Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya alitangaza siku 7 za maombolezo ya nchi nzima kufuatia kifo cha Rais John Pombe Magufuli wa Tanzania. Katika taarifa aliyoitoa jana, Rais Kenyatta ameamrisha bendera za  Kenya na Jumuiya ya Afrika Mashariki kupepea nusu mlingoti kwa muda wa siku saba. Rais Magufuli alifariki dunia Jumatano jioni Machi 17, 2021 kwa matatizo ya moyo. 

Wakati huo huo Msemaji wa Serikali ya Tanzania, Dk Hassan Abbas amesema mwili wa aliyekuwa Rais wa Tanzania, John Magufuli utaagwa katika miji mitatu ya Dar es Salaam, Dodoma, Mwanza, Geita na Chato ambako ndiko atakakozikwa.

342/