3 Septemba 2022 - 20:25
Amir-Abdollahian: Sera ya Mambo ya Nje ya Iran imejengeka katika msingi wa uhuru, amani

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema mazungumzo na utendaji wa Jamhuri ya Kiislamu katika siasa za nje umejengeka katika msingi wa uhuru, kujitegemea, amani na heshima.

Akizungumza katika kikao na wajumbe wa Jumuiya ya Kimataifa ya Ahlul-Bayt kutoka nchi 118 kinachofanyika mjini Tehran, Hossein Amir-Abdollahian amezungumzia hali iliyopo ya ulimwengu wa Kiislamu na vitisho na fursa zilizo mbele yake.

Waziri Amir-Abdollahian ametaja maandalizi ya mazingira ya kubadilishana mawazo wanazuoni wa Kiislamu duniani kuwa ni moja ya mafanikio yenye thamani ya Mkutano Mkuu wa 7 wa Jumuiya ya Kimataifa ya Ahlul-Bayt.

Ameashiria majaribio ya maadui ya kutaka kuleta mgawanyiko baina ya Waislamu na kuwasilisha taswira potovu ya kuuonyesha Uislamu kuwa ni dini ya ghasia na mapigano na kusema kuna haja ya kutilia mkazo juu ya umoja wa makundi ya Kiislamu na juhudi za kuutambulisha Uislamu wa kweli.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesisitiza kuundwa kwa makubaliano ya kimataifa dhidi ya ghasia, kwa kuzingatia mafundisho ya Kiislamu kuhusu amani na uadilifu na kufichuliwa kwa vipengele vinavyokinzana vya haki za binadamu za Magharibi.

Kongamano la Saba la Jumuiya ya Kimataifa ya Ahul Bayt (AS) mjini Tehran lilianza Alhamisi kwa hotuba ya Rais Ibrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na linatazamiwa kumalizika leo.

Kongamano hilo linajadili masuala ya vyombo vya habari, intaneti, familia, wanawake katika vyuo vikuu na uchumi. 

342/