Safari ya Amirabdollahian nchini Saudi Arabia inaweza kutajwa
kuwa hatua ya nne ya mchakato mpya wa kurejesha uhusiano kati ya Tehran
na Riyadh. Awamu ya kwanza ya uhusiano huo ilianza Machi tarehe 10 mwaka
huu. Siku hiyo, Iran na Saudi Arabia zilifikia makubaliano huko Beijing
ya kurejesha uhusiano wao wa kidiplomasia. Hatua ya pili ya uhusiano
ilikuwa safari ya wajumbe wa kiufundi wa nchi hizi mbili kwa ajili ya
kufunguliwa tena maeneo ya kidiplomasia. Hatua ya tatu ilikuwa ni
kufunguliwa kwa balozi na balozi ndogo. Hatua ya nne ya uhusiano huo
imekuwa safari za viongozi wa ngazi za juu wa kidiplomasia. Faisal bin
Farhan alitembelea Iran tarehe 17 Juni ambapo alikutana na kuzungumza na
waziri mwenzake Amirabdollahian pamoja na Rais Ebrahim Raisi.
Amirabdollahian pia alisafiri Riyadh Alhamisi Agosti 17, ambapo
alikutana na mwenzake wa Saudia, na Ijumaa akakutana na kuzungumza na
Mohammad bin Salman, Mrithi wa Kiti cha Ufalme, huko Jeddah.
Mkutano kati ya mawaziri wa mambo ya nje wa Iran na Saudi Arabia ni mkutano wao wa nne tangu kurejeshwa uhusiano wa kidiplomasia. Amirabdollahian na Faisal bin Farhan walikuwa tayari wamekwishakutana katika miji ya Beijing, Cape Town na Tehran, na mkutano wao huko Riyadh ni wa nne kwa lengo la kutekeleza makubaliano yaliyofikiwa huko nyuma.
Hii ni ziara ya kwanza ya waziri wa mambo ya nje wa Iran nchini Saudi Arabia baada ya miaka 7 ya kuvunjika uhusiano wa kidiplomasia. Pia umekuwa mkutano wa kwanza kufanyika kati ya afisa wa ngazi ya juu wa Iran na Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudi Arabia. Mazungumzo ya saa tatu na nusu kati ya Amirabdollahian na Faisal bin Farhan yanaashiria hamu ya Iran na Saudi Arabia ya kuendeleza uhusiano na ushirikiano wa pande mbili na vilevile wa kieneo. Siku ya Alhamisi Amirabdollahian alisema katika mkutano na waandishi wa habari akiwa na mwenzake Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Saudi Arabia kwamba: "Nina furaha kuwa leo tumekuwa na mazungumzo yenye tija na muhimu mjini Riyadh. Iran na Saudi Arabia ni nchi mbili muhimu katika ulimwengu wa Kiislamu. Kwa bahati nzuri, sasa uhusiano kati ya nchi hizi mbili uko kwenye njia sahihi na unaendelea kuimarika."Bin Farhan amesisitiza azma kubwa ya Saudi Arabia ya kustawisha uhusiano na Iran na kusema: "Tunatarajia kufunguliwa ukurasa mpya katika uhusiano kati ya nchi hizi mbili na ambao utafuatiliwa kwa kuzingatia udugu, kuheshimiana na maslahi ya pamoja."
Nukta nyingine ni kwamba safari na mikutano ya Amirabdollahian na viongozi wa Saudia imefanyika baada ya kikao cha maafisa wa kijeshi wa Iran na Saudia siku chache zilizopita pambizoni mwa Mkutano wa Usalama wa Moscow. Kanali ya televisheni ya France 24 kwa kuchapisha ripoti kuhusu mikutano kati ya maafisa wa kijeshi wa Iran na Saudi Arabia na ziara ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran nchini Saudi Arabia, imetathmini safari hii kuwa ni hatua mpya ya kutoa msukumo katika uhusiano wa Tehran na Riyadh.
Ingawa maelezo zaidi ya mazungumzo ya Amirabdollahian na Waziri wa Mambo ya Nje pamoja na Mwana Mfalme wa Saudia hayakutangazwa, lakini inaonekana kwamba safari ya Rais Ebrahim Raisi wa Iran nchini Saudi Arabia tayari imethibitishwa. Akizungumzia mwaliko rasmi wa Mfalme Salman wa Saudi Arabia kwa Rais Ibrahim Raisi kwa ajili ya kuitembelea nchi hiyo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudia amesema wanatarajia ziara ya Raisi nchini Saudia itafanyika hivi karibuni. Nasser Kanani, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran pia ameashiria kwamba licha ya kuwa tarehe ya kufanyika safari hiyo bado haijaainishwa lakini, Mwenyezi Mungu akipenda na kwa kuzingatia utaratibu na mipango inayofanywa, safari hii itafanyika wakati unaofaa.
342/