Siku ya Ijumaa, usitishaji vita haukurefushwa tena huko Gaza kutokana na utawala wa Kizayuni kukwamisha kwa makusudi juhudi za upatanishi na kuanzisha tena mara moja mashambulizi yake ya kinyama dhidi ya ukanda huo.
Jeshi la utawala wa Kizayuni lilianzishaa tena mashambulizi yake dhidi ya makazi ya raia katika eneo la Al-Qararah lililoko Khan Younis kusini mwa Ukanda wa Gaza na boti za kivita za utawala huo kutekeleza mashambulizi makali huko magharibi mwa mji wa Deir al-Balah. ulioko katikati mwa Ukanda wa Gaza, ambapo makombora ya utawala huo katili yamekuwa yakifanya uharibifu mkubwa katika maeneo ya magharibi mwa kambi ya Jabalia iliyoko kaskazini mwa Gaza.
Tangu kuanza tena duru mpya ya mapigano baada ya kusitishwa vita, Wapalestina wasiopungua 240 wameuawa shahidi katika mashambulizi ya utawala huo katika Ukanda wa Gaza, na wengine zaidi ya 650 wamejeruhiwa katika mamia ya mashambulizi ya anga na makombora yanayolenga makazi ya raia kwenye ukanda huo.Katika kukabiliana na mauaji ya raia wa Palestina huko Gaza, wanamuqawama wa Palestina wameshambulia miji inayokaliwa kwa mabavu ya Tel Aviv, Ashdod, Ashkelon na vitongoji vingine vya walowezi wa Kizayuni vilivyoko karibu na Gaza.
Vikosi vya Abu Ali Mostafa vimetangaza kushambulia kwa maroketi mji wa Kisofim ikiwa ni katika kujibu mashambulizi ya wavamizi dhidi ya raia wa Palestina.
Vikosi vya Al-Qassam, tawi la kijeshi la Hamas, huku vikisisitiza kulenga askari wa Kizayuni kwa ndege tatu zisizo na rubani za Zawari, vimetangaza pia kulenga idadi kubwa ya magari ya utawala wa Kizayuni kaskazini mwa eneo la kati mwa Ukanda wa Gaza.
Wapiganaji wa Hizbullah ya Lebanon pia wameshambulia kambi na vituo muhimu vya jeshi la utawala wa Kizayuni kwenye mpaka wa Palestina inayokaliwa kwa mabavu na Lebanon, kwa shabaha ya kulipiza kisasi mashambulizi yanayoendelea dhidi ya wakazi wa Gaza.
Dawood Shahab, mmoja wa viongozi wa harakati ya Jihad Islami amesisitiza kuwa, wanamuqawama wa Palestina wako tayari kwa hali yoyote ile. Mlingano wa mateka mmoja wa Israel dhidi ya wafungwa watatu wa Kipalestina unahusiana tu na raia, lakini mlingano wa kuachiliwa mateka wa kijeshi katika vita ni kuachiliwa wafungwa wote wa Kipalestina ambao wamepewa vifungo vya muda mrefu katika jela za Wazayuni.
Kwa mujibu wa jeshi vamizi la Kizayuni, hivi sasa mateka 137 wakiwemo wanawake 17 wangali mikononi mwa Hamas katika Ukanda wa Gaza. Mateka 113, wakiwemo wageni 24, tayari wameachiliwa huru katika mpango wa kubadilishana mateka.
Dhia Rashwan, Mkuu wa Idara ya Intelijensia ya Misri amesema: Misri imesikitika sana kuona muda wa usitishaji mapigano wa kibinadamu ukimalizika katika Ukanda wa Gaza na kwa sasa inafanya jitihada zake zote kwa ajili ya kurejeshwa haraka usitishaji vita mwingine.
Vyanzo vya habari katika jeshi la Israel vimesema kuwa mashambulizi ya nchi kavu yataanza katika Ukanda wa Gaza katika siku chache zijazo kwa njia ya kushtukiza.
342/