Vita vya jinai vya utawala huo vimeingia katika mwezi wake wa tisa katika Ukanda wa Gaza. Kuachiliwa huru mateka wa Kizayuni na kuangamizwa Hamas yalikuwa malengo mawili makuu yaliyotangazwa na utawala wa Kizayuni katika kuanzisha vita hivyo, malengo ambayo hakuna hata moja ambalo limefikiwa hadi sasa. Hata hivyo, swali linaloulizwa ni kuwa je, kwa nini kuna uwezekano wa utawala wa Kizayuni kuingia kwenye vita vya pande zote na Hizbullah ya Lebanon?
Sababu ya kwanza ni kwamba utawala wa Kizayuni, baada ya kushindwa katika vita vya Gaza, unakusudia kupata uzoefu wa vita vipya na hasimu wake huyo mkubwa kuliko Hamas ili kujaribu kuthibitisha kwamba bado una nguvu kubwa ya kijeshi na kwamba jeshi lake halijachoka bado kwenye medani ya vita.
Sababu ya pili kuhusiana na suala hilo ni kwamba Wazayuni wanadhani kuwa kwa kuishambulia Hizbullah ya Lebanon, Marekani italazimika kuingia kwenye vita vipya na kundi hilo la mapambano ya Kiislamu ambapo kuna uwezekano wa kushinda vita hivyo. Hata hivyo, vyanzo vya habari vimetangaza kuwa Rais Joe Biden wa Marekani amemwambia Benjamin Netanyahu Waziri Mkuu wa Israel kwamba Marekani haitashiriki katika vita vyovyote vipya iwapo utawala huo utafungua uwanja mwingine wa vita katika eneo.
Sababu ya tatu inahusiana na nafasi ya Hizbullah ya Lebanon katika vita vya sasa huko Gaza. Katika hali ambayo nchi za Kiarabu zimeamua kunyamaza kimya na kutochukua hatua yoyote ya kusimamisha mauaji ya kimbari yanayofanywa na utawala wa Kizayuni huko Gaza, Hizbullah ya Lebanon na Yemen ni wahusika wawili pekee wa Kiarabu ambao wameingia moja kwa moja vitani kwa ajili ya kuunga mkono watu wa Gaza.Kimbunga cha al-Aqsa kilifanyika tarehe 7 Oktoba, ambapo kilitoa pigo kali la kijeshi na kiusalama lisiloweza kufidika kwa Wazayuni. Utawala wa Kizayuni uliamua kuanzisha vita vikali na mauaji ya kimbari dhidi ya raia wa kawaida wa Gaza siku hiyo hiyo ya tarehe 7 Oktoba. Siku moja tu baada ya kuanza vita dhidi ya Gaza, Hizbullah nayo iliingia vitani dhidi ya utawala wa Kizayuni kwa upande wa kaskazini. Seyyed Hassan Nasrallah, Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon alitangaza kuwa Hizbullah iliamua kuingia katika vita vya Gaza mnamo tarehe 8 Oktoba. Hizbullah imekuwa ikipigana vita hivyo kwa kujidhibiti na hatua kwa hatua. Kwa maneno mengine, Hizbullah imejiepusha kuingia kwenye vita vikubwa vya pande zote na utawala wa Kizayuni ili kwa upande mmoja, kutouonyesha utawala wa Kizayuni uwezo wake wote wa kijeshi na kwa upande mwingine, iilazimishe Tel Aviv kuelekeza sehemu ya nguvu zake upande wa kaskazini. Kwa mujibu wa Sayyed Hassan Nasrallah, asilimia 30 ya vikosi vya kijeshi vya utawala wa Kizayuni vimetumwa katika eneo la kaskazini.
Huku Hizbullah ikiwasababishia Wazayuni hasara kubwa ya kibinadamu katika vita hivi, imepelekea uwezo wa kijeshi wa utawala huo kuendelea kutiliwa shaka. Kuhusiana na hilo, hivi karibuni Hizbullah iliweza kuiangusha ndege isiyo na rubani ya kisasa na ya hali ya juu ya utawala huo unaokalia kwa mabavu Quds Tukufu, inayojulikana kwa jina la Hermes 900. Kwa kuiangusha ndege hiyo, Hizbullah imethibitisha kivitendo kuwa ina uwezo wa kutumia teknolojia ya kisasa ya silaha. Ndege zisizo na rubani za Hermes 900, ambazo kwa hakika ni za kisasa zaidi za kizazi cha ndege zisizo na rubani za Hermes 450, ni miongoni mwa zana za kijeshi ambazo zinajivuniwa sana na jeshi la utawala ghasibu wa Israel. Kabla ya Hizbullah kutungua ndege hiyo, nchi kadhaa zilikuwa zimewasilisha maombi yao ya kununua ndege hizo zisizo na rubani kutoka kwa utawala wa Kizayuni.
342/