26 Juni 2024 - 17:04
CAIR: Dunia ina wajibu wa kukomesha mauaji ya watoto Gaza

Kundi la kutetea haki za Waislamu na kiraia nchini Marekani limeeleza kusitikishwa na hali mbaya ya watoto katika Ukanda wa Gaza, na kusisitiza kuwa jamii ya kimataifa na wajibu wa kusimamisha mauaji ya watoto Gaza.

Taarifa ya Baraza la Mahusiano ya Kiislamu Marekani (CAIR) inasema kuwa, Wamarekani na jumuiya ya dunia kwa ujumla wanapasa kufanyia kazi ripoti mpya ya kuogofya ya shirika la kimataifa la kutetea haki za watoto la Save the Children. 

CAIR imesema ripoti ya Save the Children inayosema kuwa, mbali na maelfu ya watoto kuthibitishwa kuuawa, wengine zaidi ya 21,000 hawajulikani walipo huko Gaza, inapasa kuiamsha dunia na kuifanya ichukue hatua za kivitendo za kukomesha jinai na chinja chinja ya watoto wa Kipalestina Gaza kwa uungaji mkono wa Marekani.

Shirika hilo la kiraia la US limesema: Mauaji ya kimbari lazima yakome, na wananchi wa Palestina sharti watazamwe kama wanadamu, sio wanyama wanaochinjwa ovyo na utawala unaofanya mauaji kimbari kwa uungaji mkono wa utawala wa (Rais Joe) Biden.Watoto 15,000 wengi wao wakiwa wanafunzi wa shule na chekechea, wameuawa shahidi huko Gaza Palestina tangu utawala haramu wa Israel ulipoanzisha hujuma na mashambulio ya kinyama katika Ukanda huo Oktoba mwaka jana.

Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF), watoto 3,000 wa Kipalestina wapo katika ncha ya kuaga dunia mbele ya jamaa zao kwa kukosa matibabu ya utapiamlo wa kiwango cha juu kusini mwa Ukanda wa Gaza. Jana Jumatatu, James Elder, Msemaji wa UNICEF alisema watoto 100 wa Kipalestina ama wanauawa au kujeruhiwa kila siku Gaza.


342/