22 Septemba 2024 - 18:43
Mlipuko mgodini waua watu 51, na kujeruhi 20 katika mkoa wa Khorasan Kusini, Iran

Zaidi ya watu 50 wamepoteza maisha na wengine kadhaa kujeruhiwa kutokana na mlipuko mkubwa uliosababishwa na uvujaji wa gesi kwenye mgodi wa makaa ya mawe katika mkoa wa Khorasan Kusini Mashariki mwa Iran.

Ripoti za vyombo vya habari zimesema kuvuja kwa gesi ya methane kulisababisha mlipuko huo katika vitalu viwili vya mgodi wa Madanjoo karibu na Tabas Jumamosi usiku, na kusababisha vifo vya watu 51 na wengine 20 kujeruhiwa kati ya karibu watu 70 wanaofanya kazi kwenye mgodi huo.

Televisheni ya taifa imeonyesha picha za magari ya kubebea wagonjwa na helikopta zikifika eneo la tukio kuwasafirisha majeruhi ili kuwapeleka hospitali.

Shirika la Hilali Nyekundu la Iran limesema shughuli za utafutaji na uokoaji zilikuwa zikiendelea katika mgodi huo lakini "mlundikano wa gesi mgodini" umefanya shughuli za utafutaji kuwa ngumu.

Rais Masoud Pezeshkian ametuma salamu za rambirambi kwa familia za wahanga na kuagiza juhudi zote zifanywe kuwaokoa waliokwama na kuzisaidia familia zao.

Pia amesema uchunguzi wa tukio hilo umeanza.

342/