Trump alitoa onyo hilo kupitia jukwaa lake la mitandao ya kijamii, Truth Social, Jumanne, baada ya waandamanaji wanaounga mkono Palestina kujitokeza nje ya Chuo Kikuu cha Columbia, New York.
Mtawala huyo wa Marekani ameandika: “Ufadhili wote wa serikali ya shirikisho utasitishwa kwa vyuo, shule au taasisi yoyote ya elimu inayoruhusu maandamano haramu."
Aliendelea kusema kuwa “wachochezi” watatiwa gerezani au kufukuzwa kabisa kurejea katika nchi walikotoka. Aliongeza kuwa wanafunzi wa Kimarekani watatimuliwa kabisa chuoni au, kulingana na uhalifu wao, watakamatwa.
Ingawa hakutaja moja kwa moja maandamano ya wanaounga mkono Palestina, Trump hapo awali alikuwa ametishia kuwafukuza Marekani wanafunzi wowote wanaoshiriki maandamano dhidi ya Israel na wanaopinga mauaji ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza.
Mwishoni mwa Januari, Trump alisaini agizo la rais linaloweka mkakati wa kuwafukuza wanafunzi wa kigeni waliopatikana wakishiriki maandamano yanayounga mkono Palestina.
Makundi ya kutetea haki na wasomi wa sheria wanasema kuwa agizo hilo linakiuka haki ya uhuru wa kujieleza inayolindwa na katiba.
Hatua hii mpya inakuja takriban wiki moja baada ya Leo Terrell, mkuu wa kikosi kazi cha Idara ya Haki ya Marekani (DOJ) kinachoshughulikia masuala ya chuki dhidi ya Wayahudi, kusema kuwa wanafunzi wanaoshiriki maandamano yanayounga mkono Palestina wanaweza kufungwa kwa miaka kadhaa.
Tangazo hili limekuja wakati ambapo wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Columbia wameanza tena maandamano mapya ya kuunga mkono Palestina, baada ya wenzao wawili kufukuzwa chuoni kwa kushiriki harakati za kupinga mauaji ya halaiki.
Vitisho vya Trump pia vimejitokeza sambamba na hotuba zilizopangwa za Naftali Bennett, aliyewahi kuwa Waziri Mkuu wa Israel, katika vyuo vikuu vya Columbia na Harvard, huku maandamano ya wanafunzi yakiendelea.
Zaidi ya waandamanaji 200 wanaounga mkono Palestina na kupinga Israel walikusanyika mbele ya Chuo Kikuu cha Columbia huko New York kupinga hotuba ya Bennett.
342/
Your Comment