7 Machi 2025 - 22:36
Source: Parstoday
Netanyahu awazidishia vizuizi Wapalestina vya kusali Ijumaa Msikiti wa Al-Aqsa mwezi wa Ramadhani

Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel Benjamin Netanyahu ameidhinisha vizuizi vikali vya kuwekewa Waislamu Wapalestina kuingia katika Msikiti wa Al-Aqsa kwa ajili ya Sala ya Ijumaa wakati huu wa mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Taarifa kutoka ofisi ya Netanyahu imeeleza kuwa utawala huo wa Kizayuni umepitisha pendekezo la kiusalama la kuruhusu idadi maalumu ya waumini kutoka Ukingo wa Magharibi kuingia Msikitini humo, kwa kuendeleza utaratibu ule ule uliotumika mwaka jana.

Chini ya vizuizi hivyo vipya, ni wanaume walio na umri wa zaidi ya miaka 55, wanawake wenye umri zaidi ya miaka 50 na watoto chini ya miaka 12 tu ndio wataruhusiwa kuingia katika Msikiti wa Al-Aqsa kwa ajili ya kusali Sala ya Ijumaa.

Hata hivyo, Waislamu walioruhusiwa wataweza kufanya hivyo ikiwa tu watapata kwanza kibali cha usalama na kufanyiwa upekuzi wa kina wa kiusalama katika vituo vilivyoainishwa.

Uamuzi huo wa kidhalimu umetangazwa sambamba na vitendo vya kishenzi vinavyoendelea kufanywa kila siku na mamia ya walowezi wa Kizayuni vya kuuvunjia heshima kwa kuuvamia Msikiti wa Al-Aqsa wakati wa mwezi huu mtukufu pamoja na kuongezwa vizuizi kwa Wapalestina kusafiri kutoka Ukingo wa Magharibi.

Tangu utawala wa Kizayuni ulipoanzisha vita vya kikatili dhidi ya Ukanda wa Ghaza Oktoba 7, 2023, mamlaka za utawala huo ghasibu zimeweka sheria kali zinazowazuia Wapalestina kusafiri kutoka Ukingo wa Magharibi kuelekea Baitul Muqaddas Mashariki.

Wakati huo huo, polisi ya utawala haramu wa Israel imetangaza kuwa inapeleka vikosi vya ziada vya usalama katika mji huo unaokaliwa kwa mabavu wakati huu wa mwezi wa Ramadhani.

Wapalestina wanavielezea vizuizi vyote hivyo kuwa ni sehemu ya njama kubwa za utawala wa Kizayuni za Kuiyahudisha Baitul Muqaddas Mashariki, pamoja na Msikiti wa Al-Aqsa, na kufuta utambulisho wake wa Kiarabu na Kiislamu.../

342/

Your Comment

You are replying to: .
captcha