Katika taarifa yake ya mapema leo Jumapili, baraza hilo limetangaza kuwa Vikosi vya Wanajeshi vya Yemen viko tayari kikamilifu kutekeleza maagizo ya Abdul-Malik al-Houthi, kiongozi wa harakati ya muqawama ya Ansarullah ya Yemen, mara tu makataa ya siku nne yatakapomalizika.
Hivi karibuni wanamapambano wa Ansarullah waliipa Israel muda wa siku nne kuhakikisha inakomesha mashambulizi yake ya kikatili dhidi ya wananchi wa Ghaza na kuheshimu makubaliano yaliyofikiwa baina yake na Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS. Makubaliano hayo yalihitimisha mashambulizi ya zaidi ya miezi 15 ya utawala wa Kizayuni dhidi ya Ukanda wa Ghaza.
Taarifa ya vikosi vya ulinzi vya Yemen imesema: "Tunathibitisha kwamba tuko tayari kikamilifu kutekeleza maagizo ya Kiongozi wa Mapinduzi ikiwa muda wa mwisho utamalizika, bila ya adui Mzayuni kukomesha mashambulizi yake. Adui Mzayuni na washirika wake ndio watakaobeba dhima kamili ya kuanza tena operesheni za majini za Yemen."
Yemen imelaani pia kushiriki kikamilifu washirika wa Israel hasa Marekani katika kuusaidia utawala wa Kizayuni, kijeshi, kisiasa na kijasusi wakati wa mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina ambapo taarifa za karibuni zinasema kuwa, Wapalestina 48,453, wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto wamethibitishwa kuuliwa kigaidi na Israel wakati wa mashambulizi ya Ghaza.
Baada ya Israel kuanzisha mashambulizi ya kigaidi dhidi ya Ghaza tarehe 7 Oktoba, 2023, vikosi vya Yemen navyo viliamua kufunga Bahari ya Sham na kuzuia vyombo vyote vya utawala wa Kizayuni na vilivyokuwa vinaelekea Israel kutumia bahari hiyo, na hivyo kuusababishia hasara kubwa sana utawala wa Kizayuni.
342/
Your Comment