Esmail Baqaei amesema kuwa, hujuma za kijeshi zinazofanywa na Marekani na Uingereza huko Yemen ni ukiukaji mkubwa wa kanuni za Mkataba wa Umoja wa Mataifa na kanuni za kimsingi za sheria za kimataifa kuhusu marufuku ya matumizi ya nguvu na kuheshimu mipaka ya ardhi na mamlaka ya nchi mbalimbali.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameyataja mashambulizi ya pamoja ya majeshi ya Marekani na Uingereza dhidi ya watu shujaa wa Yemen kuwa yanafanyika kwa sababu ya himaya na uungaji mkono wa nchi hizo mbili kwa mauaji ya kimbari yanayofanywa na Israel dhidi ya wananchi wanaodhulumiwa wa Palestina na kukandamiza aina yoyote ya mshikamano na uungaji mkono kwa haki halali za watu wa Palestina. Amesisitiza kuwa, chimbuko la ukosefu wa usalama katika eneo la Magharibi mwa Asia ni kuendelea mauaji na kukaliwa kwa mabavu ardhi ya Palestina, jambo ambalo linaendelea kwa msaada na himaya kamili wa Marekani, Uingereza na baadhi ya nchi za Magharibi, na hivyo kuweka amani na usalama wa kieneo na kimataifa katika hatari isiyo na kifani.
Esmail Baqaei amekumbusha majukumu ya kisheria na kimaadili ya nchi zote na jumuiya za kimataifa na za Kiislamu ya wajibu wa kukabiliana na mauaji ya kimbari na maangamizi ya kizazi huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu - ambayo yanatekelezwa kwa njia mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kuwatesa kwa njaa wananchi madhulumu wa Palestina katika mwezi mtukufu wa Ramadhani. Vilevile ametoa wito kwa jamii ya kimataifa kuchukua hatua za haraka kuhusiana na suala hilo.
Makumi ya watu, wakiwemo wanawake na watoto wadogo, wameuawa katika mashambulizi yanayoendelea kufanywa na majeshi ya Marekani na Uingereza dhidi ya taifa la Yemen.
Harakati ya Ansarullah ya Yemen imepa kwamba uchokozi huu hautapita bila jibu, na kwamba jeshi la nchi hiyo limejipanga kikamilifu kujibu mashambulizi hayo.
342/
Your Comment