20 Machi 2025 - 17:33
Source: Parstoday
Onyo la Iran kwa Marekani kuhusu matokeo mabaya ya uchokozi wa aina yoyote

Amir Saeed Irvani, Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa alitahadharisha katika barua yake kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa siku ya Jumatatu kwamba, hatua zozote za kichokozi zitakazofanywa na Marekani zitakuwa na matokeo mabaya na hatari mno.

Barua hii imewasilishwa kwa Baraza la Usalama kufuatia vitisho vya mara kwa mara vya hivi karibuni vya Rais Donald Trump wa Marekani na maafisa wengine wakuu wa usalama na kijeshi wa nchi hiyo dhidi ya Iran.

Baada ya kushambulia maeneo ya Ansarullah ya Yemen, Trump ameonya kuwa Iran ndiyo itakayobebeshwa lawama ya hatua ya yoyote ya kulipiza kisasi mashambulio hayo.

Karoline Leavitt, msemaji wa Ikulu ya White House, baada ya kusoma taarifa rasmi kutoka kwa Donald Trump, iliyosema kuwa mashambulizi yote ya Houthi yanahusiana moja kwa moja na Iran na kwamba ufyatuaji wowote wa kundi hilo unachukuliwa kama hatua ya Tehran, amesisitiza kuwa ni bora kumchukulia Trump kwa uzito kwa sababu yeye si kama rais aliyemtangulia.

Maafisa wengine wakuu wa usalama na kijeshi wa utawala wa Trump wamechukua msimamo sawa na huo kuhusu Iran ambapo wametishia kuishambulia kijeshi. Katika taarifa yake ya kwanza baada ya shambulio la anga la Marekani dhidi ya Yemen, ambalo lilipelekea makumi ya raia kuuawa shahidi, Pete Hegseth, Waziri wa Ulinzi wa Marekani alidai: "Enzi za kufikia amani kupitia nguvu zimerejea. Katika utawala wake wa kwanza, Trump alilazimika kukabiliana na udhaifu wa utawala wa Obama na Daesh. Sasa, anashughulikia udhaifu wa Biden. Mashambulizi haya yanatuma ujumbe wa wazi. Ujumbe wetu kwa Iran pia ni: Uungaji mkono wenu kwa Wahouthi lazima ukome, la sivyo tutakukubebesheni lawama za vitendo vya Wahouthi na wala hatutakuwa na huruma. Huu sio utawala wa Biden."

Mike Waltz, Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Marekani alirudia kauli ya Trump na vitisho vyake dhidi ya Iran siku ya Jumapili katika mahojiano na ABC ambapo alisema: "Chaguzi zote ziko mezani. Iran lazima izingatie maneno ya rais kikamilifu. Kiwango cha uungaji mkono wa Iran kwa Mahouthi, Hezbollah na makundi mengine ya wapiganaji hakikubaliki."

342/

Your Comment

You are replying to: .
captcha