Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Leo tarehe 1 Juni, 2025, baadhi ya Wanafunzi wa Madrasatul Hizbullah Al-‘Ilmiyyah (maarufu kama Bustani ya Elimu), iliyopo katika kijiji cha Kazole, kata ya Vikindu, Wilaya ya Mkuranga, Mkoa wa Pwani, walishiriki katika mtihani wa mwisho wa Mwezi kama sehemu ya tathmini ya maendeleo yao ya kielimu.
Madrasah hiyo, ambayo inalenga kuwajenga wanafunzi katika msingi imara wa elimu ya Dini ya Kiislamu pamoja na maadili mema, imekuwa nguzo muhimu ya malezi ya kijamii na kiroho kwa watoto na vijana wa eneo hilo.
Mtihani huo unafanyika kila mwisho wa Mwezi kwa lengo la kupima kiwango cha uelewa wa wanafunzi katika masomo mbalimbali kama vile Qur’an, Hadithi, Fiqhi, Tauhidi, na lugha ya Kiarabu.
Katika mtihani wa leo, walimu na wasimamizi wa madrasah walielezea kuridhishwa kwao na mwitikio wa wanafunzi pamoja na juhudi walizozionesha katika kujifunza. “Huu ni ushahidi wa bidii na nia njema ya wanafunzi wetu katika kutafuta elimu kwa ajili ya dini yao na maisha ya baadaye,” alisema mmoja wa walimu wa madrasah hiyo.
Wazazi na walezi nao wamekuwa wakitoa ushirikiano mkubwa kuhakikisha watoto wao wanahudhuria masomo kwa wakati na kujiandaa ipasavyo kwa mitihani kama hii.
Mafanikio ya Wanafunzi katika elimu ya Dini yanachangia pia kuimarika kwa jamii yenye maadili, amani, na mshikamano.
Katika kueleza umuhimu wa kujifunza, maandiko matukufu yanasisitiza thamani ya elimu, kama ilivyo katika Dua maarufu aliyokuja ndani ya Qur'an Tukufu na aliyotufunza Nabii wetu Muhammad (S.A.W.W):
"وقل رب زدني علما"
(Na sema: Mola wangu, nizidishie Elimu) - Qur’an, Surat Taha: 114.
Madrasatul Hizbullah Al-‘Ilmiyyah inatoa wito kwa jamii kuendelea kuiunga mkono taasisi hiyo ili iweze kuendelea kutoa elimu bora na kukuza kizazi chenye maarifa, hikma na hofu ya Mwenyezi Mungu.
Your Comment