22 Machi 2025 - 21:24
Source: Parstoday
Mkuu wa ujasusi Israel akiri Iran "imejipenyeza kwa kina", amlaumu Netanyahu

Kiongozi wa shirika la ujasusi wa ndani la utawala wa Israeli amesema Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ndiye anayepaswa kulaumiwa kutokana na matatizo makubwa ya utawala huo, ikiwemo usimamizi mbovu uliosababisha kile alichotaja kuwa "upenyaji wa kina" wa Iran kwenye taasisi za kiusalama na kijasusi za Israel.

"Israel inapitia kipindi kigumu na chenye changamoto nyingi," Mkuu wa Shin Bet, Ronen Bar, ameandika katika ujumbe uliolenga utawala wa Netanyahu siku Alhamisi. 

"Mkono wa Iran umo ndani kabisa ya Israel," ameongeza, akitaja hali hiyo kuwa moja ya matatizo makubwa yanayoikabili Israel.

Matatizo ambayo Bar amesema yanaukumba utawala huo yanajiri wakati ripoti za kuongezeka kwa kesi za ujasusi ndani ya utawala wa Kizayuni zinazidi kuongezeka.

Mnamo Januari, Shin Bet ilidai kuwa kesi za ujasusi kwa niaba ya Iran zilizoainishwa na huduma hiyo ziliongezeka kwa "asilimia 400" mwaka 2024 ikilinganishwa na mwaka uliotangulia. 

Ripoti hiyo ilidai kuwa imewashtaki walowezi haramu 27 kama sehemu ya uchunguzi wa kesi hizo. Shirika hilo pia lilidai kuwa limesambaratisha "operesheni 13 kubwa za ujasusi" zilizolenga utawala huo. 

Bar amemkosoa Netanyahu kwa kuweka vikwazo katika uchunguzi kuhusu kushindwa kwa taasisi za ujasusi za utawala huo, ikiwemo mianya iliyotumiwa na Harakati za Muqawama za Kipalestina mnamo Oktoba 7, 2023, kuendesha operesheni ya kihistoria katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu (Israel), ambapo walichukua mateka wengi baada ya kuingia ndani ya maeneo hayo na kuzingira kambi za kimkakati za Israel. 

Barua ya mkuu huyo wa taasisi ya ujasusi ya Shin Bet imekuja baada ya Netanyahu kuidhinisha kumfuta kazi, hatua ambayo imekosolewa sana ndani ya utawala huo kwani imetajwa kuwa yenye msukumo wa kisiasa. 

Bar amedai kuwa kuondolewa kwake kulilenga kuzima uchunguzi wa kina wa matukio ya Oktoba 7, uchunguzi ambao ungeweza kuhatarisha maisha ya kisiasa ya Netanyahu.

Maandamano yameibuka Israel, ambapo waandamanaji Wazayuni wamemlaumu Netanyahu kwa kutumia vita dhidi Gaza kama njia ya kupotosha changamoto zake za kisiasa, zikiwemo kesi za ufisadi zinazomkabili.

342/

Your Comment

You are replying to: .
captcha