Vyanzo vya hospitali vimeiambia televisheni ya Al Jazeera kwamba, Wapalestina wasiopungua 77 wakiwemo watoto wadogo wameuawa shahidi katika hujuma hizo za Wazayuni tangu alfajiri ya jana.
Msemaji wa Ulinzi wa Raia wa Gaza, Mahmud Bassal amesema makumi ya watu wamejeruhiwa pia katika hujuma hizo. Moja ya mashambulizi hayo limelenga jengo la Shirika la Umoja wa Mataifa la Wakimbizi wa Palestina UNRWA lenye kliniki ya matibabu.
Tangu Israel ivunje makubaliano yake ya kusitisha mapigano na Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina Hamas mnamo Machi 18, imeua zaidi ya Wapalestina 1,000 mpaka sasa.
Wizara ya Afya ya Gaza imesema kwa ujumla Wapalestina 50,423 wamethibitishwa kuuawa shahidi na wengine 114,638 kujeruhiwa katika mashambulizi ya Israel dhidi ya Gaza tokea Oktoba 7, 2023.
Kwa upande wake, Ofisi ya Vyombo vya Habari vya Serikali imesasisha idadi yake ya vifo hivyo hadi zaidi ya 61,700, ikisema maelfu ya watu waliofukiwa chini ya vifusi wanakisiwa kuwa wamekufa.
Wakati huo huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres ameelezea wasiwasi wake kuhusu 'gharama ya kibinadamu' ya mashambulizi ya Israeli yaliyoongezeka katika Ukanda wa Gaza.
"Katibu Mkuu amesikitishwa sana na idadi ya watu wanaokabiliwa na mapigano makali huko Gaza. Analaani mauaji yanayoripotiwa ya zaidi ya watu elfu moja, wakiwemo wanawake na watoto, tangu kuvunjika kwa makubaliano ya usitishaji mapigano," taarifa kutoka kwa ofisi ya msemaji wake imeeleza.
342/
Your Comment