Sayyid Abdul Malik Badruddin al Houthi, Katibu Mkuu wa Harakati ya Ansarullah ya Yemen amesema: "Uchokozi wa Marekani hautaathiri nguvu za kijeshi za Yemen na hautozuia operesheni za kishujaa za kijihadi za kuiunga mkono Ghaza."
Katibu Mkuu wa Harakati ya Ansarullah ya Yemen ameongeza katika ujumbe wake kwa mnasaba wa sikukuu ya Idul Fitr kuwa: Waislamu wote wanapaswa kuzingatia kwamba kuna njama kubwa za Marekani na Israel za kutaka kuangamiza kadhia ya Palestina hivyo kila mmoja ni wajibu wake kukabiliana na njama hizo.
Sayyid Abdul Malik Badruddin al Houthi
Kwa upande wake, Sheikh Naim Qassem, Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon alisema wiki hii kwamba: "Leo tunashuhudia Muqawama ambao umekita mizizi kati ya watu wa Palestina na umefanya miujiza ambayo imemtia kiwewe adui kutokana na ukakamavu na ushujaa wao wa kupigiwa mfano.”
Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon ameongeza kuwa: "Israel ni adui katili anayependa kufanya jinai na kujitanua ambaye hana mipaka bali muda wote anachupa mipaka yote.”
Sheikh Naim Qassim, Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon
Khalil al-Hayyah, mkuu wa harakati ya Hamas huko Ghaza pia amesisitiza kuwa, njama zote za adui Mzayuni dhidi ya uthabiti na irada ya wananchi wa Palestina hazitawateteresha Wapalestina. Mkuu huyo wa Hamas huko Ghaza pia amesema: "Tunashuhudia uimara huu, irada hii, na jabali hili la Palestina linalosambaratisha njama na mipango yote ya maadui." Ufahamu wa kina na uelewa wa taifa hili kubwa una uwezo wa kukabiliana na njama za maadui, udanganyifu, ukandamizaji na ugaidi wao.
Makundi ya Muqawama ya Palestina yalianzisha Operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa tarehe 7 Oktoba 2023, ili kukabiliana na jinai za utawala wa Kizayuni. Makundi ya Muqawama katika eneo hili ikiwemo harakati ya Ansarullah ya Yemen, vikosi maarufu vya kujitolea vya wananchi wa Iraq maarufu kwa jina la Hashd al Shaabi na Hizbullah ya Lebanon yalichukua hatua sambamba na mashambulizi ya jeshi la Israel dhidi ya watu wasio na ulinzi wa Ghaza kwa ajili ya kuwatetea ndugu zao wa Palestina na kupiga maeneo na vituo vingi vya kijeshi vya Israel na vituo vya usalama na kistratijia.
Operesheni ya Kimbunga cha al-Aqsa ilibadilisha mlingano wa nguvu katika eneo hili, na makundi ya Muqawama yamethibitisha kwamba propaganda za utawala wa Kizayuni na vyombo vya habari vya Marekani na Magharibi vinavyowaunga mkono Wazayuni kuhusu kutoshindwa Israel ni uwongo mtupu. Nguvu na makundi ya Muqawama zimedhihirisha wazi ukweli huo. Aidha imethibitika kwamba Israel ni tete na dhaifu sana katika vita vikubwa licha ya makeke na majigambo yake ya kila namna.
Huku vita vya Ghaza na jinai za utawala ghasibu wa Kizayuni dhidi ya wananchi wasio na ulinzi wa Palestina zikiendelea, umoja na mshikanao wa makundi ya Muqawama katika eneo hili nao umeongezeka. Makundi hayo yanaendelea na operesheni zao katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni ambazo zimepewa jina bandia la Israel, licha ya vitisho na propaganda chungu nzima za vyombo vya habari vya Magharibi.
Ujumbe wa wakati mmoja kutoka kwa viongozi wa makundi ya Muqawama katika eneo hili ni mtazamo halisi na unaoeleweka kuhusu matukio ya leo hii kwenye eneo la Asia Magharibi. Dunia nzima leo hii imeona na kujikinaisha kwamba Wazayuni kwa uungaji mkono wa moja kwa moja wa Marekani na Magharibi haujui kitu kingine isipokuwa kufanya jinai dhidi ya watoto, wanawake na raia wa kawaida. Kila mtu imemthibitikia hivi sasa kwamba njia mwafaka ya kuuzuia utawala wa Kizayuni usilete migogoro ni kutegemea uwezo wa kiutendaji na kijeshi wa makundi ya Muqawama, jambo ambalo limepelekea Wazayuni wazidi kukata tamaa.
Viongozi wa makundi ya Muqawama wanajua vyema kwamba viongozi wa utawala wa Kizayuni wanatumia kila fursa kukiuka usitishaji vita wa Lebanon na Ghaza. Kuwa macho makundi ya Muqawama huko Palestina na Hizbullah ya Lebanon kumelishangaza jeshi la Israel kiasi kwamba viongozi wa Israel wanakiri waziwazi kuwa hawana uwezo wa kukabiliana na makundi hayo ya Muqawama.
Kuendelezwa oparesheni za Yemen katika Bahari Nyekundu dhidi ya Marekani na Uingereza nchi mbili za kibeberu ambazo ni waungaji mkono wakuu utawala wa Kizayuni ni sehemu nyingine ya uwezo wa makundi ya Muqawama katika kukabiliana na mhimili wa shari wa Marekani na Israel.
Kudumishwa umoja na kutilia mkazo suala la kuunga mkono kadhia ya Palestina kumekuwa ni mafanikio muhimu zaidi ya kiroho na kisiasa ya makundi ya Muqawama katika eneo hili, jambo ambalo limekuwa na taathira kubwa katika ulimwengu wa Kiislamu na katika nyoyo za walimwengu kwa ujumla. Wazayuni wameangukia pua na uwezo mkubwa wa makundi ya Muqawama wa kujibu jinai za Israel umewashangaza. Mtazamo wa makundi ya Muqawama katika eneo hili leo hii ni kukabiliana kwa mapana na njama za utawala wa Kizayuni, na ili kufikia lengo hilo makundi hayo yameamua kushikamana katika kuunga mkono matakwa halali ya wananchi wa Palestina.
Suala jingine la uwezo wa makundi Muqawama ni kuunda uwanja mpana wa vita huko Yemen, Lebanon na Palestina na makabiliano ya moja kwa moja ya makundi hayo na utawala wa Kizayuni, jambo ambalo limezidisha pakubwa udhaifu wa Wazayuni.
Your Comment