Lavrov, ameeleza kwamba kipaumbele cha Russia ni ushirikiano katika nyanja za ulinzi na usalama, uchumi na diplomasia na kusisitiza kwamba Moscow inakutambua kuundwa Muungano wa Sahel kuwa ni jaribio la kubuni usanifu mpya wa usalama katika eneo hilo.
Russia imetangaza utayarifu wake wa kutoa msaada wa pande zote wa kiusalama kwa nchi za eneo la Sahel, wakati ambapo nchi za eneo hilo zimekuwa zikisumbuliwa na mivutano ya kisiasa, kiuchumi na kiusalama kwa muda mrefu.
Niger, Mali na Chad ni miongoni mwa nchi za eneo hilo ambazo zimekumbwa na mapinduzi na mabadiliko ya kisiasa na kijamii katika miaka ya hivi karibuni. Nchi hizo, ambazo zinasumbuliwa na ongezeka kubwa la harakati za makundi ya kigaidi, uwepo wa vikosi vya kijeshi vya Ufaransa, hali mbaya ya uchumi na machafuko ya kisiasa, sasa zinajaribu kuliko wakati mwingine wowote, kupanua uhusiano wao na nchi nyingine.
Muungano wa Mataifa ya Sahel (AES) ulioundwa na Mali, Niger na Burkina Faso mwaka 2023
Moja ya hatua muhimu zaidi za nchi za eneo hilo, haswa katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, ni vita na mapambano dhidi ya ukoloni mamboleo wa Ufaransa katika eneo la Sahel barani Afrika.
Kwa muda sasa, nchi hizi zimetaka rasmi kuondoka vikosi vya majeshi ya Ufaransa katika nchi za eneo hilo, kwa kadiri kwamba, hatimaye Paris imelazimika kukubali matakwa ya nchi hizo na kufunga kambi zake za kijeshi na kisha kuwaondoa rasmi wanajeshi wake katika nchi za eneo hilo.
Nchi za eneo la Sahel ambazo zina nafasi ya nzuri katika jiografia ya kisiasa ya Afrika, zimekuwa zikikosoa mara kwa mara sera na uingiliaji kati wa Paris katika masuala ya eneo hilo na kutangaza kwamba, haziwezi tena kuvumilia dhulma na siasa za kikoloni za Ufaransa na nchi nyingine za Magharibi. Katika muktadha huu, viongozi wa baadhi ya nchi za Kiafrika wamesema mara kwa mara kwamba: Ufaransa ina mtazamo wa dharau kwa Afrika na Waafrika, na kwamba viongozi wa Ufaransa wanapaswa kujifunza kuheshimu watu wa Afrika na kutambua thamani ya kujitolea kwao. Kwa mfano tu, Rais wa Burkina Faso, Ibrahim Traore amesema: "Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron anawadharau Waafrika wote, hatuoni sisi kuwa wanadamu."
Siasa za kiimla na za kikoloni za nchi za Magharibi hususan Ufaransa dhidi ya nchi za Kiafrika zimezifanya nchi hizo kupunguza au kuvunja uhusiano wao na Paris na kutaka kuanzisha uhusiano mpya wa kibiashara na kiusalama unaozingatia kuheshimiana na nchi nyingine.
Nchi za Magharibi, hasa Ufaransa na Marekani, ziliingia barani Afrika katika miongo ya hivi karibuni kwa ahadi za maendeleo, amani na usalama; hata hivyo uwepo wa nchi hizo barani humo umesababisha ukosefu wa amani, umaskini na kudhoofika mamlaka ya kitaifa ya nchi za Afrika.
Sasa, nchi hizi zinatafuta uhusiano wa karibu na Russia katika kalibu tofauti na kwa mtazamo unaozingatia kuheshimiana kwa pande mbili. Russia pia imetangaza utayari wake katika suala hili. Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia, Sergei Lavrov amesema: "Moscow iko tayari kutoa msaada wa pande zote kwa Muungano wa Nchi za Sahel."
Wanajeshi wa Ufaransa wakiondoka Niger
Katika miaka ya karibuni, Russia imeweza kupata nafasi kubwa katika nchi nyingi za Afrika, ikiwa ni pamoja na Mali, Burkina Faso, Jamhuri ya Afrika ya Kati na Niger, si kwa kutumia mienendo ya kikoloni ya nchi za Magharibi, bali kupitia ushiriki sawa na wenye manufaa kwa pande zote husika. Katika suala hili, utendaji wa Russia unaonyesha kuwa Moscow sio tu mshirika wa kutegemewa wa nchi za Kiafrika, bali pia mtetezi wa ulimwengu wa kambi kadhaa anayeheshimu uhuru na mamlaka ya kujitawala ya mataifa mengine. Kwa msingi huo, nchi za Sahel zimechagua kushirikiana na Russia katika nyanja mbalimbali, hasa katika masuala ya usalama.
Kuhusiana na suala hilo, Abdoulaye Diop, Waziri wa Mambo ya Nje Mali amesema: "Tunataka kuwa na ushirikiano wa kimkakati na Russia ili kuimarisha uwezo wetu wa kijeshi na kukabiliana na vitisho vya kigaidi." Waziri wa Mambo ya Nje wa Burkina Faso pia ametangaza kwamba Russia ni mshirika wa kutegemewa wa nchi hiyo, akisisitiza kuwa: "Tunaweza kupata msaada kutoka Moscow kwa ajili ya kudhamini zana za kijeshi na kutoa mafunzo kwa vikosi vya jeshi."
Rais Vladimir Putin wa Russia na viongozi wa nchi za Afrika
Mbali na sekta za masuala ya kijeshi na kiusalama, katika miaka ya hivi karibuni Russia pia imetoa misaada mingi ya kibinadamu na ufadhili wa masomo kwa watu wa Afrika na vijana wanaotafuta elimu.
Kwa kadiri kwamba, kwa mtazamo wa Waafrika wengi, Russia inaonekana kuwa ndiyo nchi inayoweza kutoa changamoto kwa ushawishi wa kihistoria wa nchi za Magharibi katika nchi za bara la Afrika na kutayarisha fursa halisi ya maendeleo kujitawala kwa nchi hizo.
Kwa kutilia maanani hayo yote, inaonekana kwamba ustawi wa uhusiano kati ya nchi za Kiafrika na Russia una nafasi maalumu katika uwanja mpya wa siasa za kimataifa. Uhusiano ambao unazingatia masuala ya usalama, uchumi na diplomasia, wenye manufaa kwa pande zote, na unaoheshimu mamlaka ya kujitawala ya kila nchi.
Your Comment