9 Aprili 2025 - 21:18
Source: IQNA
Hamas yapongeza hatua ya Umoja wa Afrika kumtimua balozi wa utawala wa Israel

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina , Hamas, imelinganisha vitendo vya utawala haramu wa Israel katika Ukanda wa Gaza na mauaji ya kimbari ya Rwanda, huku ikisifu hatua ya Umoja wa Afrika Afrika kumfukuza balozi wa utawala wa Israel kutoka mkutano maalum wa kumbukumbu uliofanyika Addis Ababa, Ethiopia.

Taarifa rasmi ya harakati hiyo ya kupigania ukimbozi wa Palestina imesema: “Hamas inapongeza msimamo wa kishujaa wa Muungano wa Afrika kwa kumfukuza balozi wa chombo cha Kizayuni [ikimaanisha Israel] kutoka katika mkutano huo, ambapo mauaji ya kimbari ya Rwanda yalijadiliwa."

Balozi Avraham Neguise alifukuzwa kutoka katika mkutano huo wa Umoja wa Afrika siku ya Alhamisi, baada ya baadhi ya nchi wanachama kupinga uwepo wake.

Taarifa ya Hamas imesema: “Hali ya kutojali na jeuri ya utawala ghasibu wa Kizayuni imefikia kilele kisichowahi kushuhudiwa, kwa kutuma mwakilishi wake katika mkutano kuhusu mauaji ya kimbari, wakati jeshi lake la kikatili linatekeleza mauaji ya kimbari mabaya dhidi ya watu wetu wa Palestina katika Ukanda wa Gaza."

Harakati hiyo pia ilitoa wito kwa mashirika ya kimataifa kutangaza kususia kwa ujumla “utawala huu wa kihalifu,” kwa lengo la kuuzuia kutumia majukwaa ya kimataifa “kusafisha jina lake na kuficha uhalifu wake,” pamoja na “kuwafikisha viongozi wake kwenye vyombo vya sheria kutokana na kuwa mikono yao imejaa damu ya watoto na raia wasio na hatia.”

Umoja wa Afrika unafanya uchunguzi kubaini ni nani alimwalika balozi wa Israel kushiriki kikao hicho.

Ni vyema kukumbusha hapa kuwa, Palestina ilikuwa nchi ya kwanza kupewa hadhi ya mwanachama mwangalizi katika Umoja wa Afrika hapo mwaka 1973, na inaungwa mkono na nchi nyingi za Afrika.

Katika miaka ya hivi karibuni, Israel imefanya jitihada kubwa za kupata uanachama wa uangalizi katika Umoja wa Afrika ili kukabiliana na ushawishi wa Wapalestina, na ilipewa hadhi ya kuwa mwangalizi mwaka 2021. Hata hivyo, Israel ilifukuzwa na kunyang'nywa hadhi hiyo kwa uamuzi wa mataifa ya Afrika kutokana na kuendelea kukalia kwa mabavu ardhi ya Wapalestina.

342/

Your Comment

You are replying to: .
captcha