Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araqchi ameitaja duru ya kwanza ya mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya Jamhuri ya Kiislamu na Marekani kuwa "chanya na yenye kuleta matumaini."
Mazungumzo hayo yalifanyika katika mji mkuu wa Oman, Muscat, jana Jumamosi chini ya upatanishi wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman, Badr bin Hamad Al Busaidi.
Araghchi na Steve Witkoff, Mjumbe Maalum wa Rais wa Marekani katika Masuala ya Mashariki ya Kati (Asia Magharibi), waliongoza duru ya kwanza ya mazungumzo hayo kuhusu miradi ya nyuklia ya Tehran yenye malengo ya amani.
Akizungumza na IRIB baada ya kumalizika mazungumzo hayo, Araghchi amesema kuwa duru inayofuata ya majadiliano hayo inatarajiwa kufanyika Aprili 19 katika ngazi hiyo hiyo.
Amesisitiza umuhimu wa kuweka msingi wa mazungumzo hayo akisema kuwa, "Ikiwa tunaweza kukamilisha msingi katika mkutano ujao ... tunaweza kuanza majadiliano ya kweli kwa msingi huo."
Mwanadiplomasia huyo mkuu wa Iran amedokeza kuwa, katika hali ambayo Oman itaendelea kuwa mpatanishi, lakini eneo la mazungumzo yajayo linaweza kubadilika.
Araghchi ameongeza kuwa, mazungumzo hayo yanalenga kuunda ajenda kwa kuzingatia ratiba ya matukio.
"Tulikubaliana kufanya duru ya pili Jumamosi ijayo, na katika kikao kijacho, tutaangazia mfumo wa jumla ambao mpango unaweza kuchukua ili kuona jinsi mchakato huu unaweza kusonga mbele," amesema.
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran amesisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu inataka makubaliano ya haki na ya heshima, na yaliyojadiliwa kwenye mazingira ya usawa.
342/
Your Comment