Araghchi amefanya mazungumzo tofauti kwa njia ya simu na mawaziri wenzake wa Misri na Kuwait, akizungumzia duru ya kwanza ya mazungumzo yasiyo ya maoja kwa moja yaliyofanyika kati ya Iran na Marekani siku ya Jumamosi. Katika mazungumzo hayo ya simu, wanadiplomasia hao wakuu wa Misri na Kuwait wamekaribisha mazungumzo hayo, wakielezea matumaini kwamba yatakuwa na tija inayotakiwa.
Sayyid Abbas Araghchi, ambaye aliongoza mazungumzo na mwakilishi wa Marekani Steve Witkoff yaliyofanyika mjini Muscat, Oman, amezungumza na Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri Badr Abdelatty na Waziri wa Mambo ya Nje wa Kuwait Abdullah Ali Al-Yahya siku ya Jumapili.
Hayo ni kwa mujibu wa ukurasa wa Telegram wa msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran.
Katika mazungumzo hayo, Abdelatty ameashiria taarifa rasmi ya Misri iliyokaribisha mazungumzo kati ya Iran na Marekani na kueleza kwamba anatumai mazungumzo hayo yataleta matokeo yanayohitajika.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Kuwait, ambaye nchi yake imetoa taarifa rasmi ya kukaribisha mazungumzo ya Oman naye pia amesema, ana matumaini kwamba mazungumzo hayo yatazaa matunda.
Wakati wa mazungumzo hayo aliyofanya kwa njia ya simu na wanadiplomasia wakuu wa Misri na Kuwait, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amebainisha msimamo wa Tehran kuhusu mazungumzo baina yake na Washington.
Mazungumzo ya simu ya Araghchi na mawaziri wenzake wa Misri na Kuwait yamejadili pia matukio mengine ya kikanda ikiwa ni pamoja na vita vya kinyama vinavyoendelezwa na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Ukanda wa Ghaza.../
342/
Your Comment