19 Aprili 2025 - 20:43
Source: Parstoday
Umoja wa Ulaya una mpango wa kupunguza kufanya biashara na Marekani

Ripoti zinaonyesha kuwa Umoja wa Ulaya unabuni mikakati ya kupambana vilivyo kwenye vita vya kibiashara vilivyoanzishwa na utawala wa Marekani unaoongozwa na Donald Trump.

Umoja wa Ulaya unaendelea na mkakati wake wa kuwa na njia za kukabiliana kivitendo na vita vya kiushuru vilivyoanzishwa na Donald Trump ikiwa ni pamoja na kuyawekea vikwazo mauzo ya baadhi ya bidhaa za Marekani kama sehemu ya kulipiza kisasi.

Habari hiyo imeripotiwa tena na vyombo vya habari vikinukuuu taarifa iliyotolewa na tovuti ya habari ya Bloomberg.

Duru za kuaminika za Umoja wa Ulaya zimenukuliwa na Bloomberg zikisema kuwa, EU inakusudia kutumia vikwazo hivyo kwa baadhi ya bidhaa za Marekani kama mkakati wake wa kupambana na utawala wa Donald Trump. Limeandika: Hatua hizi zitatumika tu ikiwa mazungumzo yanayoendelea baina ya Umoja wa Ulaya na Marekani hayatazaa matunda ya kuridhisha. Mazungumzo ya kupunguza mvutano wa kibiashara kati ya Marekani na mataifa ya Ulaya hadi sasa hayajazaa matunda.

Zaidi ya wiki mbili zilizopita, Mkuu wa Kamisheni ya Umoja wa Ulaya, Ursula von der Leyen alitaja ushuru wa Donald Trump kuwa pigo kubwa kwa uchumi wa dunia na kusema Umoja wa Ulaya uko tayari kuchukua hatua za kukabiliana iwapo mazungumzo na Washington yatashindwa.

Vyanzo vya kuaminika vimeiambia Bloomberg kwamba EU pia inafikiria kuchukua hatua nyingine, ikiwa ni pamoja na kuweka orodha ya ushuru na kuzuia manunuzi ya bidhaa za makampuni ya Marekani.

342/

Your Comment

You are replying to: .
captcha