Shirika la habari la ABNA linaripoti kuwa: Umoja wa Mataifa umesema kiasi ya wakenya 310 wameuawa na zaidi ya wengine 215,000 wamelazimika kuyahama makaazi yao mwaka huu kufuatia ghasia za kikabila kaskazini mwa nchi hiyo. Katika ripoti yake iliyotolewa hii leo, Umoja wa Mataifa umesema idadi ya watu waliouawa na kulazimika kutoroka makwao katika kipindi cha miezi sita ya kwanza ya mwaka huu, katika eneo la kaskazini mwa Bonde la Ufa nchini Kenya, ni sawa na idadi ya watu walioathirika mwaka mzima uliopita. Ofisi ya mratibu wa shughuli za kibinaadamu za Umoja wa Mataifa imesema ghasia zinazochochewa kikabila zimeendelea kusambaa katika eneo hilo la kaskazini mwa Bonde la Ufa kutokana na mizozo ya mipaka ya ardhi, wizi wa mifugo, mashambulizi ya kulipiza kisasi, kung'angania lishe ya mifugo, maji na ardhi pamoja na mizozo ya kisiasa. Maeneo yaliyoathirika zaidi ni Turkana, Baringo, Samburu, Marsabit na Isiolo.
Mwisho wa habari/ 291