Shirika la habari la ABNA linaripoti kuwa: Mwanajeshi wa Rwanda anayehudumia kikosi cha Umoja wa Mataifa cha kulinda amani Jamhuri ya Afrika ya Kati amewaua kwa kuwapiga risasi wanajeshi wengine wanne wa Rwanda kabla ya kujiua mwenyewe. Kwa mujibu wa msemaji wa wizara ya ulinzi ya Rwanda, jenerali Joseph Nzabamwita, upelelezi umeanza mara moja kufahamu sababu ya mauaji hayo. Nzabamwita amesema inaaminika kuwa askari huyo alikuwa na sababu za kigaidi, lakini akaongezea kwamba wanachunguza pia iwapo alikuwa na matatizo ya akili. Umoja wa Mataifa umepeleka wanajeshi wapatao 10,000 kulinda amani Jamhuri ya Afrika ya Kati, baada ya mzozo wa kugombea madaraka kuzuka mwaka 2013. Wanajeshi hao, mbali na kuhakikisha usalama wa raia wanasambaza pia misaada ya kibinadamu kwa watu walioathiriwa na mgogoro huo ndani ya nchi.
Mwisho wa habari/ 291