Shirika la habari la ABNA linaripoti kuwa: Kwa mara ya kwanza Shirika la kuzuia silaha za kemikali-OPCW, limesema wapiganaji wa kundi la kigaidi la Daesh walivishambulia vikosi vya Kikurdi nchini Iraq, kwa kutumia gesi ya sumu mwaka uliopita. Mwanadiplomasia amesema hizo ni silaha za kwanza za kemikali kutumika nchini Iraq, tangu kuanguka kwa Saddam Hussein. Duru za shirika hilo zimethibitisha kuwa vipimo katika maabara vimeonyesha kutumika kwa gesi hiyo ya sumu , baada ya kiasi ya wanajeshi 35 wa Kikurdi kuugua katika eneo la mapambano mwezi Agosti mwaka uliopita. Shirika hilo halijabainisha nani aliyetumia gesi hiyo, lakini mwanadiplomasia ambaye hakutaka kutajwa jina, amesema matokeo yanathibitisha kwamba silaha za kemikali zilitumiwa na kundi la kigaidi la Daesh ambalo linaungwa mkono na Uturuki, Saudia arabia, Marekani na washirika wake. Wataalamu wanadai kuwa gesi hiyo ya sumu huenda inatokea kwenye ghala la kemikali la Syria ambalo halijatangazwa au wapiganaji walifanikiwa kuzitengeneza na kufanya mashambulizi ya kemikali kwa kutumia makombora au roketi.
Hayo yote yanajiri wakati shirika la Ujasusi la Urusi lilitangaza kuwa limeona shehena za silaha za sumu zikitoka Uturuki zikipelekwa kwa kundi la kigaidi la Daesh na silaha hizo pia zilitumia dhidi ya wananchi wa Syria na kisha kutuhumiwa kuwa majeshi ya serikali ndio yalitumia silaha hizo, lakini baada ya uchunguzi kubainika kuwa serikali haijahusika vyombo vya habari vilikaa kimya kuelezea muhusika halisi wa shambulizi hilo.
Mwisho wa habari/ 291