Shirika la habari la ABNA linaripoti kuwa: Rais Barack Obama anatarajiwa leo kutoa msukumo wa mwisho kuhusu kulifunga gereza lenye utata la Marekani la Guantanamo Bay, akiwa na matumaini ya kutimiza ahadi aliyotoa wakati wa kampeni ya uchaguzi.
Ikiwa ni mwaka mmoja tu kabla ya kuacha madaraka, Obama ataweka wazi nafasi za kulifunga gereza hilo katika taarifa atakayoitoa leo.
Kiasi ya wafungwa 90 watuhumiwa wa ugaidi bado wako katika gereza hilo la Guantanamo , ambalo linauwezo wa kuwahifadhi wafungwa 700 na limekuwa eneo linalotambulika duniani kote kama eneo la mateso, kifungo bila kufikishwa mahakamani pamoja na mavazi yake ya rangi ya chungwa.
Kwa miaka kadhaa, juhudi za Obama kulifunga gereza hilo zimezuiwa na wabunge wa chama cha Republican, wengi wao wanaliona kuwa ni chombo chenye manufaa katika kupambana na ugaidi.
Mwisho wa habari/ 291