Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Rais Joko Widodo wa Indonesia amesema kuwa nchi yake inapinga vikali ukatili uliofanyika Paris nchini Ufaransa na katika mji wa Nice, lakini pia inalaani vikali matamshi yaliyotolewa na Rais Emmanuel Macron wa nchi hiyo akivunjia heshima Uislamu na itikadi za Waislamu kote duniani.
Rais wa Indonesia amesema kuwa matamshi hayo ya Macron yumkini yakazusha mpasuko baina ya wafuasi wa dini tofauti na kwamba uhuru wa kujieleza unaovunjia heshima hadhi, utukufu, thamani na nembo za kidini hauwezi kamwe kukubalika na unapaswa kusitishwa.
Joko Widodo amesisitiza kuwa, ni makosa makubwa kuhusisha dini na vitendo vya kigaidi, na kwamba magaidi hawana mfungamano na dini yoyote.
Wakati huo huo Rais Recep Tayyip Erdoğan wa Uturuki amesema kuwa wale wanaotetea vitendo viovu dhidi ya Mtume wa Mwenyezi Mungu au kiongozi wa nchi kwa kisingizio cha uhuru wa kusema na kujieleza wanavuruga na kuharibu maana ya demokrasia.
Erdoğan amesema kuwa, hatua yoyote ya kumvunjia heshima Mtume Muhammad (saw) inaulenga Umma wa Kiislamu na kwamba kushadidi uhasama dhidi ya Uislamu katika baadhi ya nchi ikiwemo Ufaransa ni ushahidi wa kuendelea kuwepo fikra potefu zilizoitumbukiza Ulaya katika maafa ya mara kwa mara.
Katika upande mwingine Askofu Mkuu wa mji wa Toulouse nchini ufaransa, Robert Jean Louis Le Gall amesema kuwa, anapinga uhuru unaobeza na kudhalilisha dini na vilevile anapinga kitendo cha kuchapisha vibonzo kama vile vinavyomvunjia heshima Mtume Muhammad (saw).
Matamshi hayo ya Askofu Mkuu wa Toulouse yametolewa baada ya hujuma iliyopelekea kuuliwa watu watatu katika kanisa la mji wa Nice na baada ya kuuliwa mwalimu aliyewaonesha wanafunzi wake vibonzo vinavyomvunjia heshima Mtume Muhammad (saw).
Robert Jean Louis Le Gall amesisitiza kuwa haijuzu kuruhusu watu kuchezea shere na kuzivunjia heshima dini za Mwenyezi Mungu.
Juzi pia Waziri Mkuu wa Canada Justin Trudeau alijitenga tena na mienendo ya Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa ya kuhalalisha na kutetea matusi na kuvunjiwa heshima itikadi na matukufu ya Uislamu kwa kisingizio cha "uhuru wa kusema na kujieleza" na kusisitiza kwamba, uhuru huo una mipaka yake.
Amesisitiza kuwa uhuru wa kusema na kujieleza unapaswa kutumiwa kwa hadhari.
Waziri Mkuu wa Canada, Justin Trudeau amesema kuwa gaidi aliyetekeleza hujuma ya kigaidi katika mji wa Nice nchini Ufaransa hawakilishi dini ya Uislamu wala Waislamu, na kwamba watu wote wanapasa kukiri ukweli huo.
Hata hivyo Justin Trudeau amesisitiza kuwa, watu wa aina hii hawawakilishi dini ya Uislamu.
Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa amekuwa akitetea hatua ya jarida la Charlie Hebdo la nchi hiyo la kuchapisha tena vibonzo vinavyomtusi na kumvunjia heshima Mtume muhammad (saw) akitaja kitendo hicho kuwa ni "uhuru wa kujielweza"!
342/